Thursday, 6 July 2017

WALIOCHAPISHA PICHA ZINAZODAIWA KUMKASHIFU RAIS KUPANDA KIZIMBANI AGOSTI 3

Image result for mahakamani

Kesi ya kusambaza taarifa za uongo kwenye mtandao ya kijamii ya WhatsApp Juni 9, 2016, inayowakabili wanafunzi wanne wa Chuo Kikuu cha Kampala (Kiu), kampasi ya Dar es Salaam imeahirishwa hadi Agosti 3, mwaka huu.

Wanafunzi hao wanadaiwa siku hiyo ya tukio, walichapisha picha ambazo zinamuonyesha Rais John Magufuli akiwa amevaa hijabu kama mwanamke wa Kislamu na kuzisambaza kwenye mitandao, huku wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Pia, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kutengeneza picha hizo kwa kutumia kompyuta na baadaye kuzisambaza kwenye WhatsApp kwa lengo la kumuudhi na kumkashifu Rais

Kesi hiyo iliyopo katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imeahirishwa leo (Alhamisi, Julai 6) baada ya wakili wa upande wa mashtaka Florida Wenceslaus kutokuwepo mahakamani.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Amenitha Kongo (19), Maria Tweve (20), Agnes Gabriel(21) na Anne Mwansasu(21).

“Mheshimiwa hakimu, kesi hii imekuja leo kwa ajili ya kusikilizwa na washtakiwa wote wapo mbele ya mahakama yako, lakini wakili anayeendesha shauri hili hayupo hapa mahakamani hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuanza kusikiliza,” amedai wakili Silyvia Mitanto.

Kwa upande wake, wakili wa utetezi, Peter Kibatala ameiomba Mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo, Agosti 3, mwaka huu maombi ambayo yalikubaliwa na Mahakama.

Hakimu Mkazi anayesikiliza shauri hilo, Catherine Kiyoja alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na la upande wa utetezi na kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 3, mwaka huu itakapoanza kusikilizwa ushahidi.Reactions:

0 comments:

Post a Comment