Tuesday, 4 July 2017

TUNDU LISSU AINYAMBUA MISWADA YA MADINI

Image result for tundu lissu

Anaandika Tundu Lissu

Leo Bunge linajadili Muswada wa marekebisho ya sheria za madini na za kodi katika sekta ya madini.

Makampuni ya kigeni ambayo yametunyonya tangu miaka ya mwisho ya ’90, na yanaendelea kutunyonya hadi sasa, hayapo kwenye mjadala huu.

Acacia Mining PLC, ambayo Magufuli na maprofesa wake wamedai imetupiga zaidi ya shilingi trilioni 139 wakati haina hata leseni ya uchimbaji madini, nayo haipo kwenye mjadala huu.

Kama nilivyotabiri mwezi uliopita, Magufuli amesalimu amri mbele ya makampuni haya na mbele ya Acacia Mining PLC.

Naomba kufafanua.
Muswada unaojadiliwa leo umetamka wazi kuwa mikataba ya uendelezaji madini iliyopo sasa itaendelea.

Hii ni pamoja na mikataba ya Acacia Mining PLC kuhusu Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara. Kwa Muswada huu, mikataba hii ni halali.
Kusalimu amri huku kwa Magufuli kuna maana kubwa sana.

Mjadala wa makinikia ya dhahabu sasa ndio umezikwa rasmi.

Kama mikataba ya Acacia Mining PLC ni halali, maana yake ni kwamba usafirishaji wa makinikia ulikuwa halali muda wote. Watayarudishiwa makinikia yao kimya kimya.

Sidhani kama tutamsikia mtukufu Rais wetu akizungumzia makinikia tena. Na mtakaong’ang’ania tuyajadili mtaanza kutishwa ili mnyamaze.

Hayo matrilioni ya akina Prof. Mruma na Prof. Osoro ndio hatutayasikia tena. Yalikuwa ni ya uongo, ‘professorial rubbish’, tangu mwanzo.

Ndio maana hata wabunge wameambiwa Taarifa za hao wasomi wabobezi ni mali ya Rais peke yake. Wengine haturuhusiwi kuziona.

Kama mikataba ni halali kwa mujibu wa Muswada wa leo, maana yake nyingine ni kuwa waliohusika kuiandaa au kuisaini hawana kosa lolote.

Hoja ya kuwashtaki akina Chenge, Ngeleja, Muhongo na wengineo waliotajwa kwa majina na Kamati ya Prof. Osoro, nayo sasa ni marehemu.

Kama mikataba ni halali watakamatwa na kushtakiwa kwa kosa gani???

Kwa hiyo, kwenye signature issue yake kubwa juu ya rasilmali zetu, huyu anayeitwa mtetezi wa wanyonge na mlinzi wa rasilmali zetu, ameshindwa vibaya. Magufuli ameshindwa, kama nilivyosema atashindwa.

Kwa Muswada huu, Magufuli ameendeleza na kuhalalisha matendo ya watangulizi wake Mkapa na Kikwete ya kugawa rasilimali zetu kwa wageni.

Kwa Muswada huu, waliotunyonya na kutuibia juzi na jana na wanatuibia leo, wataendelea kutunyonya na kutuibia kesho na kesho kutwa.

Muswada wa leo unafanya mabadiliko makubwa ya kisheria kwa makampuni yatakayokuja miaka ijayo.

Sawa kabisa. Lakini naomba Magufuli na wapambe wake watusaidie hili: hivi ni sehemu gani ya nchi yetu ambayo ina madini na hayana mwenyewe tayari???

Ni sehemu ipi ya eneo letu la bahari au eneo maalum la kiuchumi ambalo bado halina mikataba ya kutafuta au kuchimba mafuta au gesi asilia???

Nchi hii ilishagawanywa vipande vipande na kupewa wawekezaji wakati wa Mkapa na Kikwete.

Muswada huu ni mzuri kwenye karatasi, kiuhalisia sheria yake haitatekelezeka kwa sababu mali tayari ilishauzwa na Muswada huu umebariki biashara hiyo.

Magufuli na watu wake hawataki watanzania wajue hili. Ndio maana Muswada unaletwa kwa dharura, ili kusiwe na mjadala wowote wa kina.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment