Monday, 10 July 2017

TRA IRINGA YASHIKIRIA MAGARI YANAYODAIWA KODI ILIYOFUTWA

Image result for JENGO LA TRA IRINGA

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Iringa inaendelea kuyashikilia magari waliyoyakamata kwa kosa la kutolipa ada ya mwaka ya leseni ya magari kabla haijafutwa na serikali; ikisubiri waraka wa serikali utakaoleza utaratibu wa kuyaachia.

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake jana, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, ambao kikodi unahusisha na mkoa wa Njombe, Lamson Tulyanje alisema magari hayo yapo katika vituo mbalimbali katika wilaya za mikoa ya Iringa na Njombe.

Alitoa ufafanuzi huo baada ya baadhi ya walipa kodi kulalamika kwa wanahabari wa mjini Iringa kwamba baadhi ya maafisa wa TRA wa mjini Iringa wamekuwa wakiwadai ada hiyo pamoja na kwamba serikali imeifuta.

“Kuna ofisa mmoja alinidai ada hiyo nilipokwenda wiki iliyopita kuchukua cheti cha mlipa kodi (certificate) baada ya kulipa kodi ya kuuza ardhi,” alisema mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina moja la Kindimba..

Alisema afisa huyo (hakumtaja jina) alimwambia hawezi kupata cheti hicho mpaka atakapolipa ada ya leseni ya magari yake ambayo ni zaidi ya Sh Milioni 5.

“Kwahiyo nimekosa cheti hicho ambacho ni cha lazima katika mchakato wa kubadili umiliki wa ardhi ambayo familia yetu imeuza kwasababu nadaiwa ada ya leseni ya magari ambayo serikali imetangaza kufuta,” alisema.


Kindimba alisema baada ya mabishano na afisa huyo alielezwa kwamba amuone meneja au asubiri waraka wa maelekezo ya kufutwa kwa kodi hiyo.

Akijibu madai hayo, Kaimu Maneja wa TRA mkoa wa Iringa alisema mlalamikaji huyo atakuwa na jambo la ziada analoficha katika maelezo yake na si kweli kwamba anatakiwa kupewa cheti hicho kwa sharti la kulipa ada hiyo.

“Toka serikali ilipotangaza kufuta ada hiyo, hatukusanyi na hatuakusanya kwa mtu yoyote ada hizo na kila mtumishi wa TRA ana maelekezo hayo,” alisema.

Alisema ada ya mwaka ya leseni ya magari ilikuwa ikiuungizia mkoa wa Iringa na Njombe zaidi ya Sh Milioni 800 kwa mwezi lakini baada ya kufutwa mapema Juni mwaka huu, mapato hayo yalishuka hadi zaidi ya Sh Milioni 200.

Alisema wapo walipa kodi wanaodaiwa kodi zingine zikiwemo za mapato na uhamishaji wa umiliki wa magari lakini wamekuwa wakizihusisha kodi hizo na ada ya mwaka ya leseni ya magari ambayo kimsingi ndiyo iliyofutwa.


Aliwataka wenye malalamiko hayo kufika ofisini kwake na kumuona yeye moja kwa moja ili wafuatilie taarifa zao na kujua changamoto zipo wapi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment