Monday, 10 July 2017

TANESCO YATATHMINI MATUMIZI YA NGUZO ZA UMEME ZA ZEGE


SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limesisitiza azma yake ya kutumia nguzo za umeme za zege ikiwa ni hatua mojawapo ya kuboresha huduma ya usambazaji na upatikanaji wa umeme nchini.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na HabariLeo hivikaribuni mjini Iringa, Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Usambazaji wa Huduma kwa Wateja, Joyce Ngahyoma alisema kwasasa wanaendelea na utafiti wa umadhubuti wa nguzo hizo.

“Tunafanya utafiti kujua uimara wake, uzalishaji wake na usafirishaji wake. Zipo baadhi ya nchi zimeanza kutumia nguzo hizo na hapa nchini wenzetu wa TTCL wanatumia nguzo hizo,” alisema.

Alisema kama watafikia uamuzi wa kutumia nguzo hizo wataangalia uwezekano wa kuzalisha kikanda ili kurahisisha usafirishaji wake.

“Na niwahakikishie wazalishaji wa nguzo za umeme za miti kwamba hawataarhiriwa kama uamuzi wa kutumia nguzo za zege hutafanywa kwasababu mahitaji ya nguzo nchini ni makubwa sana,” alisema.

Alisema kwa wastani Tanesco wanahitaji nguzo zaidi ya 500,000 kila mwaka, kiwango ambacho soko la ndani limeshindwa kutosheleza.

“Kuna wakati tulilazimika kuagiza nguzo kutoka nje ya nchi kwasababu ya changamoto hiyo; wito wetu kwa wazalishaji wa ndani, waongeze uzalishaji ili kutosheleza mahitaji na wazingatie ubora unaotakiwa na shirika,” alisema.

Alisema shirika limejiwekea lengo la kuunganisha wateja wapya zaidi ya 250,000 kila mwaka na kwa hesabu hiyo mahitaji ni makubwa kwasababu wengine wanahitaji nguzo zaidi ya moja ili wafikiwe na huduma.

“Na ikumbukwe tunaingia awamu ya tatu ya miradi ya REA, lengo la serikali ni kuona ifikapo mwaka 2025 vijiji vyote nchini vinakuwa na umeme,” alisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment