Friday, 7 July 2017

PAMS WALIVYOWEZESHA VITA YA UJANGILI NCHINI

Image result for ujangili

VITA dhidi ya ujangili imezidi kuimarika kutokana na juhudi za serikali na wadau mbalimbali, ikiwemo kikosi kazi maalumu kilichoteuliwa kwa ajili ya kukabiliana na uhalifu huo sambamba na utoroshaji wa nyara za serikali.

Kubanwa kwa majangili kumewezeshwa na kazi nzuri inayofanywa na kikosi hicho maalumu ambacho kuanzia mwaka 2014 kimekuwa kikipigwa jeki na wapenda mali asili ikiwemo shirika la Protected Area Management Solutions (PAMS).

PAMS Foundation ni taasisi ambayo inasaidia kutoa suluhu katika kulinda na kuhifadhi mali asili katika hali bora inayokubalika.

Taasisi hii imewawezesha maofisa wa serikali wa kitengo cha National & Transnational Serious Crimes Investigation Unit (NTSCIU) kufika maeneo mengi ambayo awali hawakuweza kufika ili kufanya uchunguzi na kuongoza ukamataji wa wahalifu wanaojihusisha na nyara za serikali, hususani meno ya tembo.

PAMS kwa kuona mafanikio ya sasa imesema kwamba serikali imekuwa ikifanya vyema katika vita yake dhidi ya majangili na wasafirishaji wa meno ya tembo.

Katika miaka ya karibuni, pamoja na watu wengi kukamatwa, kutiwa nguvuni kwa raia wa China maarufu kama malkia wa meno ya tembo, Yang Feng Glan, ni tukio lililoonesha nguvu mpya katika kupambana na ujangili nchini.

Aidha kukamatwa kwa mtuhumiwa mwingine, Li Ling Ling ambaye alidakwa muda mfupi kabla ya malkia Yang kutiwa nguvuni nako kunatoa picha kwamba vita inayoendelea dhidi ya majangili siyo ya mchezomchezo.

Pamoja na kudorora kwa juhudi za kupambana na ujangili katika miaka ya nyuma (kabla ya 2014) kulikotokana na kiasi kidogo cha fedha kilichokuwa kinatengwa kukabiliana na uwindaji haramu, juhudi za PAMS Foundation ziliwezesha kupatikana kwa fedha za kusaidia mapambano haya muhimu.

Fedha hizo zilisaidia wachunguzi wanaoongozwa na kikosi kazi kilichoundwa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika mradi maalumu wa kulinda tembo kutanua wigo wa uendeshaji wa shughuli zao.

Kuanzia Oktoba 2014 shughuli za kikosi hicho zimetanuliwa na matokeo yanaonekana hasa kwa kukamatwa kwa mapapa ya ujangili.

Kuna matunda makubwa ya kuridhisha ya mradi huu wa kukabiliana na ujangili unaoendeshwa na NTSCIU.

Mafanikio hayo ni pamoja na kukamatwa kwa majangili zaidi ya 870 wakiwamo pia watu wanaofanya biashara za meno ya tembo kwa magendo.

Halikadhalika, bunduki 320 na magari 20 yaliyokuwa yakitumika katika ujangili yamekamatwa pia.

Kikosi kazi hiki mpaka sasa kimewakamata watu zaidi ya 250 kwa uvushaji nyara za serikali katika jiji la Dar es Salaam pekee akiwamo huyo aliyepachikwa jina la malkia wa meno ya tembo pamoja na Boniface Matthew Mariango, maarufu kama shetani.

Aidha ushindi wa NTSCIU unaonekana pia kwenye kesi zilizofikishwa mahakamani ambapo watu 240 wamepatikana na hatia na wako waliofungwa kwa miaka 20 na wengine chini yake.

Imeelezwa kuwa kitendo cha kurejeshwa nchini kwa Gakou Fodie kutoka Uganda kuja kujibu tuhuma za kujihusisha na uhalifu wa kimataifa wa nyara za taifa ni moja ya hatua muhimu zinazoonesha pia mafanikio katika vita dhidi ya ujangili nchini.

Fodie anatakiwa kusaidia upelelezi wa kadhia kadhaa za kimataifa ambazo yeye ametajwa kuhusika moja kwa moja ikiwamo usafirishaji haramu wa meno ya tembo.

 “Pamoja na kuhusishwa na usafirishaji wa tani sita za magamba ya kakakuona kupeleka bara la Asia kutoka Afrika, mtandao wa kimataifa wa utoroshaji wa nyara ambao Fodie anatuhumiwa kuhusika nao pia unachunguzwa, ikiwa ni pamoja na uhusiano wake na uvushaji wa meno ya tembo kwa mwaka 2015, 2016 hadi 2017,” anasema Wayne Lotter wa taasisi ya PAMS.

Kazi kubwa iliyofanywa na NTSCIU katika upelelezi na ukamataji katika mifumo kadhaa ya ikolojia imewezesha majangili kubanwa kila kona badala ya eneo moja, kama ilivyokuwa inafanyika awali kutokana na upungufu wa fedha.

Si ujangili tu bali kazi za kikosi hiki zimewezeshwa pia kukamatwa kwa magogo yaliyokuwa yanasafirishwa nje.

Kutokana na juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali chini ya serikali, uhalifu katika misitu na mbuga mbalimbali nchini unaelezwa kupungua kwa kiasi kikubwa.

“Hayo ni matokeo ya utendaji wa hali ya juu wa Kikosi kazi maalumu cha kupambana na ujangili nchini kinachounganisha kitengo cha kukabiliana na uhalifu wa kimataifa (NTSCIU) na kikosi kazi cha kukabiliana na uhalifu wa misitu na wanyamapori chini ya Wizara ya Mali Asili na utalii,” anasema Mkurugenzi wa PAMS Foundation, Krissie Clark.

Mmoja wa watendaji wanaoshirikiana NTSCIU, mwanasheria Yamiko Mlelakano pia ameleta mafanikio makubwa katika siku za karibuni za kukabiliana na uhalifu wa kwenye mbuga na misitu.

Clark anasema mwanasheria huyo amepata mafanikio katika mashauri takribani 31 aliyoyasimamia katika mahakamani ya Simiyu ambapo wahusika walitupwa jela baada ya kupatikana na hatia.

Clark anasema yeye na taasisi yake na wafadhili wa taasisi hiyo isiyo ya kiserikali wanashukuru sana kwa namna wanavyoisaidia serikali ya Tanzania kukabiliana na ujangili, hatua ambayo imechangia sana kupunguza mauaji ya tembo.

Mkurugenzi wa shirikisho la wenye hoteli nchini ambaye anashughulika na maeneo ya utalii, Malcolm Ryen, naye anakiri ujangili umepungua sana na kwamba ulikuwa unatishia hata biashara yao ya hoteli za kitalii kama tembo wangelitoweka.

Ryen anapongeza kazi nzuri iliyofanywa na NTSCIU, kikosi kazi na taasisi ya PAMS.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment