Monday, 24 July 2017

MWENYE MTOTO MWENYE MAUMBILE YA SIRI YASIYOELEWEKA AOMBA MSAADA


MSICHANA wa miaka 19, Elizabeth Chengula anaelezea anavyoishi maisha ya shida ambayo ni pamoja na kupata mtoto ambaye awali ilidhaniwa ni wa kiume lakini siku zinavyokwenda hajulikani ni wa jinsi gani baada ya maumbile yake ya siri kuwa hayaeleweki ni ya kike au ya kiume.

Chengula alisema Agosti mwaka jana alijifungua mtoto huyo katika Zahanati ya Ifisi iliyoko Mbalizi Mbeya Vijijini.

 “Kipindi chote hicho mimi namlea kama mtoto wa kiume kwa mavazi na jina nimempa la kiume, sasa nikiambiwa ni wa kike sijui nitaenda kuwaambia nini watu kule nyumbani, nadhani nitahama kabisa na sijui nitaenda wapi maana hawatanielewa,” alibainisha huku akiomba msaada utakaoleta ufumbuzi wa tatizo hilo.

Daktari Bingwa wa Upasuaji kwa Watoto, Zaituni Dkhary akizungumzia tatizo hilo, alisema mzazi yeyote anaweza kupata mtoto wa namna hii na kwamba tatizo hilo sio mkosi kwa kuwa lina ufumbuzi.

Alisema madaktari wanaofanya upasuaji wa tatizo hilo ni madaktari bingwa wa upasuaji wa watoto (Pediatric Surgeon) au madaktari bingwa wa upasuaj wa njia ya mkojo (Urologist Surgeon) na kama kuna kesi ngumu wanaweza kusaidiana lakini upasuaji huo ni wa kawaida kabisa.

Daktari huyo alisema watoto ambao wanazaliwa wakiwa na maumbile hayo ni vigumu kuelewa jinsia yake kwa kumtazama kwa macho katika sehemu zake za siri kwani wanakuwa na viungo vya jinsia ya kike na pia ya kiume.

“Watoto hawa kwa mzazi hata mzalishaji inakuwa ni vigumu kutambua kwa kuangalia kwa sababu ukimuangalia mtoto sehemu zake za siri anakuwa na kiungo cha kiume na pia maumbile ya kike na kwa chini anakuwa na tundu la kukojolea,” alieleza.Reactions:

0 comments:

Post a Comment