Friday, 7 July 2017

MTANDAO WA AGA KHAN KUJENGA CHUO KIKUU BORA MKOANI ARUSHA

Image result for Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan

Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) umeanza mchakato wa kujenga Chuo Kikuu cha Aga Khan, kampasi ya Arusha kilichoelezwa na Mkurugenzi wa AKDN, Profesa Joe Lugalla kwamba ana uhakika ndicho kitakachokuwa bora hapa Tanzania.

Chuo hicho kwa mujibu wa mtandao huo, kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 2,000 kwa mwaka.

Profesa Lugalla alisema jana kwamba ujenzi wa chuo hicho mkoani Arusha utakamilika ndani ya miaka mitano na kitaajiri kati ya watu 8,000 na 10,000.

“Chuo hicho kitakuwa cha kipekee kwa sababu kitakuwa na mazingira mazuri ya wanafunzi kusomea na kuishi. Nina uhakika kitakuwa ndiyo chuo bora hapa Tanzania,” alisema.

Profesa Lugalla, ambaye pia ni mkuu wa Chuo Kikuu cha Aga Khan (Aku), alisema mazungumzo kati ya chuo hicho na Serikali yanaendelea, na ujenzi wake ambao utagharimu mabilioni ya fedha utaanza muda wowote

Alisema chuo hicho kitadahili wanafunzi kutoka nchi mbalimbali watakaosoma kuanzia shahada ya awali mpaka ya uzamivu, lakini fursa zaidi itatolewa kwa wanafunzi watanzania.

Pamoja na mchakato wa ujenzi huo, mtandao hupia, umeanza kujenga taasisi ya maendeleo ya elimu ya Afrika Mashariki itakayokuwa na makao makuu yake jijini Dar es Salaam.

Taasisi hiyo itatoa mafunzo ya ualimu ngazi ya shahada ya uzamili kwa wanafunzi kutoka nchi za Afrika Mashariki.

Mbali na mradi huo, AKDN inatoa huduma mbalimbali kama vile za afya, kilimo na mikopo kwa wananchi ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea.

Zaidi ya wakulima wadogo 100,000 na vikundi 9,200 vya akiba na mikopo vilivyopo kusini mwa Tanzania vinanufaika na miradi inayoendeshwa na AKDN nchini.

Mtandao huo unaendesha miradi sehemu mbalimbali barani Afrika na Asia na kutoa fursa kwa watu wenye kipato cha chini kushiriki katika uzalishaji ili kujikwamua kiuchumi.

Waziri Mkuu kuhudhuria sherehe Wakati huohuo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 60 tangu Mtukufu Aga Khan alipochaguliwa kuwa Imamu Mkuu wa madhehebu ya Ismailia ulimwenguni.

Sherehe za maadhimisho hayo zitafanyika Jumapili, zikiambatana na gwaride maalumu litakaloandaliwa na jumuiya ya Waismailia wa Tanzania.

Akizungumzia sherehe hizo, mratibu wa kikosi kazi cha maandalizi, Karim Kanji alisema sherehe zitakuwa ni maandalizi ya mwaka wa Diamond Jubilee ambao utaanza Julai 11.

Kanji alisema ujio wa Waziri Mkuu kwenye maadhimisho hayo ni ushahidi wa uhusiano wa muda mrefu ambao umekuwapo kati ya Serikali na jumuiya ya Waismailia kupitia Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan, katika kusimamia maendeleo ya Taifa.

Julai 11, 1957, Aga Khan akiwa na umri wa miaka 20, alichaguliwa na babu yake kuwa Imamu wa 49 wa madhehebu ya Ismailia.


Waislamu wa Shia Imam Ismailia, ambao wanafahamika zaidi kama Waismailia, wanapatikana kwenye nchi zaidi ya 25 duniani hasa Asia

Reactions:

0 comments:

Post a Comment