Monday, 24 July 2017

LIPULI FC YAPATA VIONGOZI WAPYA, WACHEZAJI WAITWA NYUMBANI


WACHEZAJI wa klabu ya Lipuli FC ya mjini Iringa waliokuwa jijini Dar es Salaam wakiendelea na mazoezi ya maandalizi ya Ligi Kuu inayotarajiwa kuanza mwezi ujao, wameitwa mjini Iringa ili kuendelea na maandalizi yao.

Hatua hiyo imekuja baada ya klabu hiyo iliyokuwa imegubikwa na mgogoro wa uongozi wa muda mrefu kufanya uchaguzi wa viongozi wake wapya jana.

Uchaguzi huo uliosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Asia Abdalah.

Katika uchaguzi huo uliofanyika katika mazingira tulivu tofauti na matarajio ya watu wengi, Ramadhani Mahano alichaguliwa kuwa Mwenyekiti akibeba mikoba ya mwanamichezo maarufu mkoani hapa Abou Changawa Majeki aliyekuwa kiongozi wa klabu hiyo kwa miaka minne.

Mahano aliikwaa nafasi hiyo baada ya kupata kura 103 dhidi ya Nuhu Muyinga aliyepata kura 60 na Abnel Mrema aliyepata kura nne.

Aidha mkutano huo wa uchaguzi, ulimchagua kwa kura 116 Ayubu Kiwele kuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo baada ya kukosa mpinzani.

Pamoja na viongozi hao, wanachama 172 wa klabu hiyo walioshiriki katika mkutano huo wa uchaguzi walimchagua Renatus Kalinga, Sylivester Kanyika, Magid Matola na Shabani Rushino kuwa wajumbe wa kamati ya utenadaji ya Lipuli FC katika kipindi cha miaka minne ijayo.

Akishukuru kwa kuchaguliwa kuiongoza klabu hiyo, Mahano alisema kambi ya timu hiyo iliyokuwa ikiendelea jijini Dar es Salaam kwa usimamizi wa baadhi ya wadau wa mpira wa miguu mkoani Iringa itahamishiwa mjini Iringa.

“Tutafanya taratibu za kuwaleta wachezaji wetu wote mjini Iringa, tunataka Jumanne au Jumatano wawe wamerejea na wafanye maandalizi kwa ajili ya mechi ya kirafiki na Azam FC,” alisema.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kilolo alitoa wito kwa wadau wa mchezo huo kutoa ushirikiano kwa viongozi wapya watakaochaguliwa kuiongoza klabu hiyo.


 “Watu wamechoka na kelele za Lipuli za muda mrefu. Uchaguzi huu umefungua ukurasa mpya wa maendeleo ya timu na sekta zingine ikiwemo ya utalii katika mkoa wetu,” alisema huku akiwataka viongozi hao kuvunja makundi yote ya uchaguzi na kuwa kitu kimoja.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment