Monday, 10 July 2017

HANS POPE ALIPIGA JEKI JESHI LA ZIMAMOTO IRINGA
MDAU wa maendeleo ya mkoa wa Iringa, Zakaria Hans Pope ametoa msaada wa gari aina ya Mercede Benz lenye tanki la ujazo wa lita 5,000  kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Iringa.

Akikabidhi gari hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza mjini Iringa jana, Hans Pope aliahidi kutoa msaada mwingine wa gari la kubeba wagonjwa kwa jeshi hilo  huku akisema litakuja hivikaribuni.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto Tanzania (CGF) Thomas Andengenye, Hans Pope ambaye ni mmoja wa viongozi wa klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam alisema; "ataangalia pia uwezekano wa kusaidia vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuzima moto baada ya kuelezwa mapungufu yaliyopo."

Akikiri kujivunia uenyeji wake wa mkoa wa Iringa alisema ameamua kusaidia Jeshi la Zimamoto kwakuwa si utamaduni wa watu wengi wenye uwezo kutoa msaada katika jeshi hilo.

Akishukuru kwa msaada huo Mkuu wa Mkoa wa Iringa alimpongeza Hans Pope akisema ni mdau wa kweli wa maendeleo ya mkoa wa Iringa na amekuwa akisaidia sekta mbalimbali pindi anapoomba kufanya hivyo.

“Baada ya kupokea gari hili kazi iliyo mbele yetu ni kuhakikisha linatunzwa na kutumika kwa shughuli zilizokusudiwa,” alisema Masenza.

Awali CGF Andengenye alisema jeshi hilo linahudumu kwa dharula zote zinazolenga kuzuia na kupunguza idadi ya vifo, majeraha kwa watu, uharibifu wa mali unaosababishwa na moto, mafuriko, matetemeko ya ardhi, ajali za barabarani na majanga mengineyo.

Alisema mbali na majukumu hayo jeshi hilo linakabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya kuzimia moto na maokozi likiwa na magari 72 tu mazima yanayofanya kazi hiyo nchi nzima.

“Magari hayo hayatoshelezi kutoa huduma ipasavyo na mengi kati yake yapo katika hali chakavu na isiyoridhisha yakiwa na umri wa zaidi ya miaka 30,” alisema.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Iringa, Kennedy Komba alisema msada wa gari hili unafanya mkoa wa Iringa wenye vituo vya zimamoto vinne kati ya sita vinavyohitajika uwe na magari mawili baada ya moja kupata ajali hivikaribuni.

Akizungumzia takwimu za matukio ya moto na maokozi mkoani Iringa, Komba alisema mwaka 2015/2017 kulikuwa na matukio 110 na mwaka 2016/2017  kulikuwa na matukio 97.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment