Monday, 10 July 2017

DC ASIA ATAKA WANANCHI WAFICHUE MAJANGILI WANAOZUNGUKA HIFADHI


MKUU wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah amewataka wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Mazingira ya Asili Kilombero kuwafichia wanavijiji wenzao wanaoshirikiana na majangili kuhujumu hifadhi hiyo.

Mhifadhi  mkuu  wa hifadhi hiyo, Elia  Mndeme  alisema hifadhi hiyo yenye  ukubwa wa hekta 134,511   ilipandishwa hadhi kuwa  hifadhi ya  mazingira ya  asili Agosti 17, 2007  na kutangazawa kuwa eneo la urithi wa dunia katika milima ya Tao la Mashariki.
.
Alisema hifadhi  hiyo imetokana na muungano wa misitu ya hifadhi tatu ambayo ni Matundu, Lyondo na  West Kilombero scarp iliyopo katika wilaya mbili za Kilolo mkoani Iringa na Kilombero mkoani Morogoro.

Mndeme alisema kumekuwepo na vitendo vya ujangili wa miti na wanyama wadogo wanaopatikana katika hifadhi hiyo vinavyofanywa na majangili wanaoshirikina na baadhi ya wananchi wa vijiji 21 vinavyoizunguka.

Abdallah ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Kilolo alisema hifadhi hiyo inayopita katika kata za Udekwa na Ukwega wilayani mwake ni moja katika ya vivutio vizuri vya utalii wilayani humo.

 Akiwa pamoja na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya katika kata ya Udweka hivikaribuni, Abdallah alisema ni wajibu wa kila mwananchi anayeishi jirani na hifadhi hiyo kushirikiana na mamlaka zinazohusika kufichua na kupambana na ujangili.

Alisema katika kukabiliana na ujangili zipo doria shirikishi zinazofanywa na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS),, Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa (UMNP), Kikosi cha Kuzuia Ujangili (KDU), askari mgambo wa vijiji (VGS) na kamati za mazingira za vijiji (VNRCs).

Katika kuhamasisha utalii wa ndani kwa kupitia hifadhi hiyo, alisema wilaya yake inawakaribisha wawekezaji wenye uwezo wa kujenga miundombinu ya hoteli ili kuwavutia pia watalii wa nje.

Akizungumzia fursa ya uwekezaji katika wilaya hiyo, Mkurugenzi  mtendaji  wa halmashauri hiyo, Aloyce Kwezi alisema halmashauri yake ina maeneo ya kutosha yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji.

“Pia halmashauri yetu ina ardhi na maji ya kutosha kwa ajili ya kilimo cha kawaida na cha umwagiliaji. Mnakaribishwa,” alisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment