Tuesday, 4 July 2017

BULEMBO ABADILI GIA ANGANI, KUWANIA TENA UENYEKITI WAZAZI

Image result for bulembo

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Abdallah Bulembo amechukua fomu juzi mjini hapa kutetea wadhifa wake katika uchaguzi wa ndani ya chama hicho, miezi michache baada ya kutangaza asingewania nafasi hiyo.

Bulembo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM alikabidhiwa fomu na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Dodoma, Gama Juma juzi, huku akielezwa kuwa ametii shinikizo lililokuwa likitolewa na wazee, viongozi na wanachama wa jumuiya hiyo kumuomba agombea tena nafasi yake.

Mwanasiasa huyo ambaye pia alikuwa mwanamichezo maarufu nchini, alichukua fomu hizo kimyakimya kwenye ofisi za Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dodoma, tofauti na ilivyozoeleka ambako baadhi ya wawania uongozi husindikizwa na wapambe na waandishi wa habari.

Licha ya kwenda kimyakimya, lakini taarifa zilieleza kwamba Mbunge huyo wa Kuteuliwa, alifika kwenye ofisi hizo za Wazazi Mkoa wa Dodoma saa nane mchana akijiendesha kwa gari lenye namba T888 DFB aina Toyota Land Cruiser lenye vioo vya giza, na kukabidhiwa fomu hizo na mwenyekiti Juma. Bulembo alilithibitishia gazeti hili jana kwamba ni kweli amechukua fomu hiyo, lakini hakutaka kuingia undani wa suala hilo.

Mapema mwaka huu, Bulembo alitamka katika katika moja ya vikao rasmi vya jumuiya hiyo kwamba hatagombea tena nafasi yake, kauli iliyodumu kwa muda mrefu, lakini baadaye baadhi ya wazee akiwemo Balozi Job Lusinde na viongozi na wanachama wa jumuiya hiyo walitoa kauli za kumsihi abatilishe uamuzi wake huo wa kutogombea.

Maombi hayo yaliripotiwa kutolewa kwa nyakati na sehemu tofauti nchini wakiwemo makatibu wa jumuiya hiyo kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar, ambao kwenye semina moja iliyofanyika mjini hapa, mwezi uliopita, walimsihi Bulembo kuchukua fomu huku wakisisitiza kwamba ikibidhi watamlipia fedha za fomu hizo.

Kutokana na mwaka huu kuwa mwaka wa uchaguzi wa viongozi ndani ya CCM na jumuiya zake ikiwemo hiyo ya Wazazi Tanzania na Jumuiya za Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT), UVCCM kuanzia ngazi ya Tawi hadi Taifa, CCM ilitangaza kuanza kutolewa fomu kwa wanaohitaji ridhaa za uongozi kwa ngazi hizo, kuanzia juzi.

Kulingana na msimamo wa sasa wa CCM baada ya mabadiliko makubwa iliyofanya Dodoma, ambayo pamoja na kutaka kuwa na viongozi wenye nia za dhati na wenye kuguswa na shida za wananchi, bila shaka wanaowania uongozi katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huo watalazimika kujipima vya kutosha kulingana na sifa zilizotajwa.

Juzi, CCM Mkoa wa Dodoma ilianza kutoa fomu za uchaguzi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye chama na jumuiya na kusisitiza kuwa watoa rushwa hawatakuwa na nafasi ya kukiongoza chama hicho.

Akizungumzia mchakato wa uchaguzi katika ngazi mbalimbali za chama hicho, Katibu wa CCM Mkoa Dodoma, Jamila Yusuph alisema fomu hizo ambazo zitatolewa bure zitatolewa na kurudishwa ndani ya siku tisa kuanzia jana hadi Julai 10, mwaka huu.

Nafasi ambazo zinawaniwa kwa upande wa chama ngazi ya mkoa ni Mwenyekiti wa Mkoa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM ya Taifa, wagombea watakaowania nafasi 30 za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, wajumbe wawili kila wilaya wa Mkutano Mkuu wa Mkoa na Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa


Reactions:

0 comments:

Post a Comment