Thursday, 29 June 2017

WAZALISHAJI WA NGUZO ZA UMEME WATAKIWA KUZINGATIA UBORA
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limezitaka kampuni zinazojishughuliza na uuzaji wa nguzo kuzingatia viwango vya ubora kama zinataka kuendelea kufanya biashara na shirika hilo.

“Kuanzia sasa hatutakuwa tayari kuzipatia tenda kampuni zinazouza nguzo zilizo chini ya kiwango,” alisema Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Usambazaji wa Huduma kwa Wateja, Joyce Ngahyoma. 

Ngayoma aliyasema hayo mjini Iringa juzi kwenye warsha ya kimataifa ya siku tatu iliyoyokuwatunanisha watengenezaji na wasambazaji wa nguzo kutoka ndani na nje ya nchi kwa uratibu wa Tanesco na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Alisema lengo la warsha hiyo ya kimataifa ni kuhakikisha nguzo zote zinazouzwa hapa nchini zinakuwa na ubora utakaoziwezesha kudumu kwa zaidi ya miaka 40. 

Alisema  hatua hiyo imekuja baada ya shirika kubaini kuwepo na baadhi ya wauzaji , kusambaza nguzo zenye kiwango cha chini jambo linalosabisha zioze na kukatika kabla ya wakati na hivyo kulitia shirika hilo hasara ya fedha nyingi.

Alisema shirika limekuwa likitumia zaidi ya Sh Bilioni 220 kwa mwaka kununua nguzo na imekuwa ikiongeza na kulitia hasara shirika pale zinapoharibika katika kipindi kifupi na kulazimika kuzibadilisha.

Kwa upande wake Meneja wa Afya na Usalama Kazini wa shirika hilo, Mhandisi Majige Mabula alisema shirika limelenga kutoa huduma ya kiwango cha juu kwa watu wake kwahiyo ni lazima wazingatie ubora.

“Tunataka tuwe na uelewa wa pamoja  juu ya aina ya nguzo na ubora tunaouhitaji…kitaalamu nguzo zikishachimbiwa chini zinatakiwa kudumu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40,”alisema. 

Mabula alisema ubora wa nguzo unategemea aina ya mti, namna ya kupanda na kuutunza, umri wake, uvunaji, utengenezaji na kiwango cha dawa inayotakiwa kuchanganywa ili isioze.

Naye Mhandisi wa Miradi wa REA, Jensen Mhavile alisema nchi haiwezi kufikia lengo lake la kuwa taifa la viwanda kama katika sekta hiyo ya nishati kutakuwa na matumizi ya bidhaa zisizo na viwango.

Alisema hadi sasa REA imekwishasambaza umeme katika vijiji 4,395 huku matarajio yao yakiwa kusambaza umeme katika vijiji vyote 12,268 ifikapo mwaka 2021 kwa ubora unaotakiwa. 

“Utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya III umeanza kwa wakandarasi kuanza kupatiwa amikataba na tunatarajia katika awamu hii vijiji 3,559 vitapata umeme na vile vitakavyobaki vitapatiwa umeme kati ya 2018/2019 na 200/2021,”alisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment