Monday, 5 June 2017

WANAFUNZI IRINGA WANYWESHWA MAZIWA ASAS


KAMPUNI ya maziwa ya Asas imeikarimu shule ya msingi Ipogolo kwa kutoa maziwa kwa wanafunzi wake wote pamoja na msaada wa majaketi kwa wanafunzi wanaotoka familia duni ili wayatumie kujikinga na baridi.

Msaada huo ulitolewa jana shuleni hapo wakati kampuni hiyo kwa kushirikiana na wadau wake mbalimbali wa maziwa wa mkoa wa Iringa ikiungana na watanzania wengine nchini kuadhimisha wiki ya maziwa.

Maadhimisho ya wiki ya maziwa Kitaifa yaliyokwenda na kauli mbiu ya ‘kunywa Maziwa Furahia Maisha’ yalifanyika mjini Bukoba mkoani Kagera kuanzia Mei 28 hadi Juni 1, 2017.

Mwalimu  mkuu msaidizi wa shule hiyo ya Ipogolo, Makrina Mpogole pamoja na kuishukuru  kampuni ya Asas  kwa  kutoa maziwa kwa wanafunzi wote  shuleni  kwake, na majaketi kwa wanafunzi  wanaotoka familia zisizo na uwezo  alisema:

“Wazazi na walezi wa wanafunzi hao wana wajibu wa kuwawezesha watoto wao kupata paketi moja ya maziwa kila siku kabla ya kwenda shule.

Pamoja na kwamba wengi wao wana umri mdogo, mwalimu huyo alisema wana mashaka baadhi ya wanafunzi wao wanashiriki vitendo vya ulevi kwa kunywa pombe aina ya Ulanzi baada ya masomo.

Alisema baadhi ya wanafunzi hao ni wale ambao matokeo yao shuleni sio mazuri na afya zao zinaonekana kutetereka kwasababu ya matumizi ya pombe hiyo.

Meneja  wa miradi wa kampuni ya  Maziwa ya Asas, Hassan Swedi  alisema maadhimisho ya mwaka huu yamewalenga zaidi vijana hasa wanafunzi wa shule za msingi za mjini Iringa na ndio sababu  kampuni yake  imelazimika  kutoa msaada  wa maziwa na majaketi kwa  wanafunzi  wanaotoka katika familia duni .

Alisema kuwa kampuni hiyo inaamini kuwa iwapo shule zitaweka utaratibu wa kutoa maziwa kwa wanafunzi afya zao zitakuwa bora na kiwango cha uelewa na ufaulu kinaweza kuongezeka zaidi.

Alisema maadhimisho ya Wiki ya Maziwa yalianzishwa yakiwa na lengo la kuelimisha wananchi na umma juu ya matumizi ya maziwa kama chakula bora kwa watu wa rika zote na faida za maziwa katika kujenga afya ya binadamu na kukuza uchumi wa nchi.


Alisema maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kuongeza idadi ya Unywaji Maziwa nchini kutoka wastani wa lita 47  hadi lita 200 kwa mtu kwa mwaka kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Reactions:

0 comments:

Post a Comment