Thursday, 8 June 2017

VITAMBULISHO VYA TAIFA VYAANZA KUTOLEWA MANISPAA YA IRINGA


MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa imeanza zoezi la kutambua na kusajili wakazi wa Manispaa ya Iringa.

Akizungumza na wanahabari jana, Ofisa Habari wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Denis Gondwe alisema zoezi hilo limeanza juzi, Juni 7 na linatarajia kukamilika Julai 7, mwaka huu.

Alisema zoezi hilo linalohusisha usajili wa wananchi wote raia wa Tanzania wenye miaka 18 na kuendelea linafanyika katika vituo vya usajili vilivyopo katika kata zote 18 za Manispaa ya Iringa.

“Zoezi linaanza saa moja asubuhi hadi saa 11 jioni na linafanyika kwa kuzingatia ratiba ilivyopangwa ambapo kila kata imepangiwa siku tatu za usajili,” alisema.

Kwa kupitia ratiba hiyo, Gondwe alisema kata ya Ruaha na Kitwiru zimeanza zoezi hilo jana na linatarajiwa kukamilika kesho Juni 9.

Alisema kata ya Igumbilo, Mshindo, Kitanzini na Mivinjeni zitaanza zoezi hilo Juni 10 hadi 12, kata ya Mlandege, Kwakilosa na Ilala itakuwa Juni 13 hadi 15 na kata ya Mwangata na Isakalilo itakuwa Juni 18 hadi 20.

Kata ya Mkwawa itafanya Juni 21 hadi 23, kata ya Makorongoni na Gangilonga itakuwa Juni 24 hadi 26 na kata ya Kihesa Juni 27 hadi 29.

Gondwe alisema katika kata ya Mtwivilla na Mkimbizi zoezi litafanyika Juni 30 hadi Julai 2 na kata ya Nduli itakuwa Julai 3 hadi 5.

Wanapokwenda kujisajili, Gondwe alisema wananchi wanatakiwa kuwa na nyaraka halisi na vivuli vya kuthibitisha uraia na umri wa mhusika.

“Nyaraka hizo ni pamoja na cheti cha kuzaliwa, pasi ya kusafiria, vyeti vya elimu ya msingi na sekondari, leseni ya udereva, kitambulisho cha Bima ya Afya au kitambulisho cha mpiga kura,” alisema.

Alisema kwa kuwa zoezi hilo linahusisha upigaji wa picha; ili kupata picha bora wananchi wanatakiwa kutovaa nguo nyeupe, kijivu, bluu mpauko, pinki, nguo zenye kung’aa sana, jezi, nguo zenye nembo, kofia aina yeyote ama kupaka hina mikononi.

“Matarajio katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ni kusajili wakazi 130,000 kwa ajili ya Vitambulisho vya Taifa,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment