Tuesday, 27 June 2017

UCHAGUZI WA VIONGOZI WAPYA LIPULI FC WAIVA


BAADA ya danadana za muda mrefu, hatimaye imefahamika wazi kuwa, Uchaguzi Mkuu wa Klabu ya Soka ya Lipuli ya mjini Iringa utafanyika Agosti 5, mwaka huu na tayari mchakato wa kuelekea kwenye zoezi hilo umetangazwa kuanza leo.

Akizungumza na wanahabari jana, Mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) Jeremiah Wambura alisema, uchaguzi wa Lipuli FC utasimamiwa na kamati ya uchaguzi ya TFF.

Awali uchaguzi huo ulikuwa ufanyike Mei 29, mwaka huu lakini ukasitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchama wa klabu hiyo waliodai majina yao yaliondolewa kutoka kwenye leja la klabu.

Wambura alitaja nafasi zitakazogombewa kuwa ni Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ambazo fomu zake zinatolewa kwa Sh 200,000.

“Na nafasi za wajumbe watano wa kamati ya utendaji ambazo fomu zake zinatolewa kwa Sh 100,000,” alisema.

Alisema Juni 28 hadi 30 zimetengewa kwa ajili ya wagombea wa nafasi hizo kuchukua na kurudisha fomu za kuomba uongozi.

Alisema kati ya Julai 1 na Julai 30, yatafanyika mambo mbambali ikiwemo kikao cha mchujo, kutangaza orodha ya wagombea, kupokea na kupitia pingamizi, kufanya usaili, kukata na kutoa maamuzi ya rufaa za kimaadili na dhidi ya kamati ya uchaguzi na kutangaza orodha ya mwisho ya wagombea.

Alisema kampeni kwa ajili ya uchaguzi huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa soka wa mkoa wa Iringa zitaanza Julai 31 had Agosti 4.

Alisema wagombea wanatakiwa kuwa na kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne na wagombea kwa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti  ni lazima wawe na uzoefu mzuri katika uendeshaji wa mpira wa miguu kwa miaka mitano na zaidi uliothibitishwa.

TFF imetangaza uchaguzi huo wa Lipuli FC ikiwa ni siku moja baada ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo Annastazia Wambura kuliagiza Baraza la Michezo nchini (BMT) kutoa agizo kwa klabu hiyo kuhakikisha inafanya uchaguzi wake.

 

Wambura alikuwa mjini Iringa juzi kuzindua mashindano ya mpira wa miguu ya Ritta Kabati Challenge Cup yanayoshilikisha timu 10 zilizofuzu hatua ya pili ya mashindano hayo yaliyoshirikisha timu 46 kutoka wilaya zote za mkoa wa Iringa.

 

Katibu wa Lipuli FC Wille Chikweo alisema uchaguzi huo unafanyika kwa baraka zote za uongozi wao unaokaribia kumaliza muda wake.


 

Reactions:

0 comments:

Post a Comment