Wednesday, 7 June 2017

SHERIA YA USIMAMIZI WA MALIASILI YAKISAIDIA KIJIJI CHA KIWELE KUONGEZA MAPATOMAPATO yatokanayo na misitu katika kijiji cha Kiwele wilayani Iringa mkoani Iringa yanadaiwa kuongezeka baada ya Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) kuwasaidia kukamilisha mchakato wa kupata sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili hiyo.

Mchakato wa kupata sheria hiyo inayolenga kukabiliana na uharibifu wa misitu na ujangili wa wanyamapori ulifanywa na kijiji hicho mapema mwaka huu.

Afisa Mradi wa LEAT wa wilaya ya Iringa, Musa Mnasizu alisema mchakato  wa kupata sheria hiyo umefanyika kupitia mradi wao wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili unaotekelezwa katika vijiji 32 vya wilaya za Iringa na Mufindi mkoani Iringa.
  
“Lengo la mradi ni kuzijengea uwezo jamii zinazoishi karibu na rasilimali misitu na wanyamapori ili waweze kuzisimamia na kunufaika nazo kwa kuwapa mafunzo ya sheria, sera miongozo, kanuni na ufuatiliaji uwajibikaji jamii,” alisema.

Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Aloyce Shirima alisema kabla ya sheria hiyo wananchi na wageni walikuwa wakiingia katika msitu wa hifadhi wa kijiji na kufanya uharibifu mkubwa huku wakipewa adhabu ndogo.

Shirima alisema msitu wa hifadhi wa kijijini hapo ujulikanao kwa jina la Kidundakiyavi (mlima uliochimbwa) una ukubwa wa hekta 4,900, sehemu yake ikiwa imeharibiwa vibaya kutokana ujangili.

Katibu wa Kamati ya Maliasili ya kijiji hicho, Pascal Luvanda alisema kabla ya sheria hiyo, kijiji kilikuwa hakinufaiki vya kutosha na rasilimali hiyo.

“Hata yale makusanyo yaliyokuwa yanatokana na adhabu kwasababu ya uharibifu na ujangili katika msitu huo yalikuwa hayafiki Sh Milioni moja kwa mwaka,”  

Luvanda alisema kwasasa kijiji kinanufaika na ushuru unaotokana na uokotaji wa kuni kwa matumizi ya majumbani na ukataji wa miti katika sehemu iliyoruhusiwa kwa ajili ya kukaushia tumbaku.

Alisema tangu wakamilishe mchakato wa sheria hiyo, makusanyo yameongezeka kutoka Sh 900,000 zilizokuwa zikikusanywa kwa mwaka, miaka iliyopita hadi Sh Milioni tano ndani ya robo ya kwanza ya mwaka huu.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Yustini Pesambili alisema ulinzi wa msitu huo limekuwa jukumu la kila mwananchi na ndio sababu kuna manufaa hayo.


“Msitu unalindwa na wananchi wenyewe kwa kupitia kamati yao ya maliasili na chochote kinachotolewa ndani yake kinatolewa kwa kuzingatia sheria, vinginevyo kuna adhabu zake,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment