Wednesday, 21 June 2017

SHEIKH CHALAMILA AOMBA MUDA ZAIDI WA MAFUNZO YA DINI MASHULENI

Image result for SHEIKH ABUBAKARI CHALAMILA

SHEIKH wa Mkoa wa Iringa, Abubakar Chalamila ameiomba serikali kutoa muda wa kutosha wa mafunzo ya dini mashuleni akisema hatua hiyo itasaidia kurejesha maadili yanayoporomoka miongoni mwa jamii.

Aliyasema hayo juzi jioni wakati akizungumza na waumini wa dini ya kiislamu, viongozi mbalimbali na wageni wengine aliowaalika kwa ajili ya Futari aliyoiandaa katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCU), mjini Iringa.

Sheikh Chalamila alisema wizi wa rasilimali za umma, ufisadi, uzinzi, ulevi, ukwepaji wa kodi na maovu mbalimbali yanayoendelea kujitokeza katika jamii msingi wake ni ukosefu wa elimu bora ya malezi kwa watoto.

“Msingi wa malezi bora kwa watoto ni mafundisho ya dini kwani hayo ndiyo yanayozungumzia maadili na ndiyo yanayowafanya watu wawe na hofu ya Mungu,” alisema.

Alisema kwa bahati mbaya muda wa mafunzo ya dini uliopangwa mashuleni ni finyu hatua inayowafanya wanafunzi wengi ambao ni taifa la kesho kujiingiza katika vitendo vingi vinavyokiuka maadili.

“Katika shule nyingi hapa kwetu Iringa, tunapata vipindi viwili tu vya dakika 40 kila wiki, muda ambao tunadhani hautoshi na unapaswa kuongezwa ikiwezekana kipindi kimoja kila siku kwa kila darasa,” alisema.

Akishukuru kwa Futari hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamuhuri William alisema Taifa linapita katika changamoto kubwa na akaomba watanzania waunge mkono jitihada za Rais Dk John Magufuli za kupambana na maovu mbalimbali nchini.

“Ndoto ya Rais wetu ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kwa kutumia rasilimali zake iwe na uwezo pia wa kutoa misaada kwa mataifa mengine,” alisema.

Alisema ndoto hiyo haiwezi kufikiwa kama watanzania hawataunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano za kubadili mifumo ya nchi.

Kuhusu ombi la kuongezwa kwa mafunzo ya dini mashuleni, alisema; “nimepokea ombi hilo na nitalifikisha kunakohusika na kwa kuzingatia kwamba serikali inatambua mchango wa taasisi za dini katika kukuza jamii yenye maadili.”Reactions:

0 comments:

Post a Comment