Thursday, 1 June 2017

SERIKALI KUPAMBANA NA WAFANYABIASHARA MATAPELI

Tokeo la picha la waziri wa fedha

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema serikali itaendelea kutengeneza mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji nchini lakini pia kamwe haitowavumilia wafanyabiashara matapeli, wanaokwepa kodi na wale wanaoiba rasilimali za nchi.

Pamoja na hayo, amesema ni wajibu na haki kwa viongozi wenye dhamana ya kulinda rasilimali za nchi kwa niaba ya wananchi, kusema ukweli pale wanapoona kuna tatizo na wala lengo si kutishia au kuwakimbiza wawekezaji au wafanyabiashara.

 Kuhusu kilio cha wabunge cha kutekelezwa kwa ahadi ya kutolewa kwa Sh milioni 50 kila kijiji, amesema kwa sasa serikali inaandaa utaratibu unaofaa kwa ajili ya kutoa fedha hizo, ili kutorudia makosa yaliyojitokeza katika utolewaji wa fedha za mabilioni ya JK (Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete) zilizokuwa na lengo kama fedha hizo za vijijini.

 Akijibu hoja za wabunge 79 waliochangia kwenye mjadala wa kupitisha makadirio na mapato ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18 jana, Dk Mpango alisema dhana ya kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara ni jambo muhimu kwa kuwa hata serikali inatambua wazi kuwa sekta binafsi ndio injini ya uchumi wowote ule.

 Alisema serikali na sekta binafsi ni vitu vinavyofanana kama mapacha walioungana, na endapo wasipofanya mambo yao kwa mapatano ni wazi kuwa mambo yao ya muhimu hayatoweza kwenda kama inavyotarajiwa.

“Kwa muktadha huo ili kuwa na mafanikio kwa pande zote, lazima yawepo majadiliano kuhusu malengo, vipambele, sera na mikakati ya taifa letu,” alisema na kuongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inaboresha mazingira ya biashara nchini na ndio maana Rais John Magufuli alipoingia madarakani, jambo la kwanza alilolifanya ni pamoja na kukutana na wafanyabiashara.


 “Lakini pia mimi na Waziri mwenzangu wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji (Charles Tizeba) tuliitisha mkutano na wafanyabiashara hapa Dodoma na tumekubaliana tutakuwa tunakutana kila baada ya miezi minne,” alieleza

Reactions:

0 comments:

Post a Comment