Friday, 23 June 2017

SERIKALI IMESIKIA KILIO CHA WAKULIMA WA VINYUNGU IRINGA

Image result for Januari Makamba Iringa

SERIKALI imesikia kilio cha wabunge wa majimbo mbalimbali ya mkoa wa Iringa waliotaka wananchi wanaolima vinyungu katika mabonde yenye kuhifadhi unyevunyevu wasibuguziwe mpaka maamuzi ya pamoja yatakapofanyika.

Kwa nyakati tofauti katika bunge linaloendelea, wabunge wa mkoa wa Iringa waliungana na wabunge wa majimbo mengine nchini wakiitaka serikali isitishe mpango wa kuwaondoa wakulima katika maeneo hayo.

Wakiongozwa na Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi wabunge hao walitaka Serikali kusitisha zuio la kulima vinyungu mpaka tafsiri ya umbali wa mita 60 kutoka vyanzo vya maji itakapofafanuliwa ipasavyo.

Akizungumza na wadau mbalimbali wa halmashauri zote za mkoa wa Iringa katika kikao kilichoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza mjini Iringa jana Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Januari Makamba alisema;

“Zimejitokeza changamoto ya utekelezaji wa maelekezo ya kikosi kazi hicho kilichoundwa na Makamu wa Rais kwa lengo la kunusuru ikolojia ya Mto Ruaha Mkuu ambao vyanzo vyake vya maji vipo mkoani Iringa, Njombe na Mbeya.

Alisema kuna bugudha zimejitokeza hasa kwa wakulima wa vinyungu wakati maelekezo hayo yakitekelezwa jambo lililolazimisha kifanyike kikao cha muafaka baina ya viongozi wenu na wataalamu wa wizara yangu.

Alisema kati ya sasa na mpaka watakapofikia maamuzi ya pamoja wananchi wanaolima katika maeneo hayo wasibughudhiwe lakini wasiruhusiwe kuingia maeneo mapya.

Makamba alisema halmashauri zote za mkoa wa Iringa zinatakiwa kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji wa maelekezo hayo, na ihakikishe miti yote isiyorafiki na vyanzo vya maji ikiwemo mikaratusi illiyopo katika vyanzo vya maji inakatwa.

Alisema katika kufikia maamuzi serikali itatembea mkoa mzima wa Iringa, kinyungu kwa kinyungu na bonde kwa bonde kabla ya kutoa maelekezo yatakayosaidia kwa nia njema kunusuru mazingira. 

Wakitoa maoni yao baada ya maelekezo ya waziri, wabunge wa mkoa wa Iringa walisema suala la vinyungu ni la maisha kwa wananchi wengi wakulima wa mkoa wa Iringa.

“Kilimo cha vinyungu kina tija kwa wananchi wengi wa jimbo la Kalenga na mkoa wa Iringa, kimebadili maisha ya watu wengi na kimewasaidia sana. Jambo la msingi tulime sambamba na kulinda mazingira yetu na vyanzo vya maji” alisema Mbunge wa Kalenga Godfrey Mgimwa.

Naye Mbunge wa Mafinga Mjini Chumi alisema wakazi wa Iringa wanasifika kwa utunzaji wa mazingira, kinachotakiwa kufanywa ni kuelekezwa namna ya kutunza vyanzo vya maji bila kuathiri shughuli zao za uchumi.

Pamoja na Chumi na Mgimwa, wabunge wengine waliokuwepo wakati maelekezo hayo ya waziri yakitolewa ni Mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto na wabunge wa viti maalumu mkoa wa Iringa CCM, Rita Kabati na Rose Tweve waliosema tathimini ya kutosha inatakiwa kufanyika katika kilimo hicho.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment