Monday, 12 June 2017

SABA WATIWA NGUVUNI TUKIO LA MACHIMBO YA DHAHABU ISIMANI IRINGA


Jeshi la polisi mkoani Iringa linawashikiria watu 7 kwa tuhuma za kushiriki katika tukio la kuvamia na kujeruhi wachimbaji wadogo wa madini katika mgodi wa Nyakavangala uliopo Tarafa ya Ismani, wilayani Iringa na kupora mamilioni ya fedha.

Katika tukio hilo lililotokea usiku wa Juni 9, mwaka huu, watu tisa walijeruhiwa vibaya, na zaidi ya Sh Milioni 81, gramu 400 za dhahabu na simu za mikononi ziliporwa.

Akitoa taarifa kwa wandishi wa habari leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi alisema mara baada ya kupokea taarifa hizo jeshi la polisi lilifanya oparesheni ya kuwasaka watuhumiwa hao.

“Mpaka sasa tayari tumefanikiwa kuwatia nguvuni watuhimiwa saba wakiwa na Bastola moja inayosadikika ilitumika katika uvamizi huo,” alisema.

Alisema katika tukio hilo, majambazi hao walivamia machimbo hayo, na kuwalazimisha wachimbaji wadogo waliokuwepo walale chini.

“Pamoja na kuamriwa kulala chini walishambuliwa kwa nyndo na nondo jambo lililosababisha watu tisa wajeruhiwe  vibaya wakati wakijaribu kujinasua kutoka kwa majambazi hao,” alisema.

Alisema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Katika tukio lingine Kamanda Mjengi alisema jana majira ya saa 3.00 usiku shimo mojawapo la wachimbaji wadogo wa madini lilititia na watu wanne kufikiwa.

Alisema watu watatu kati yao waliokolewa na jitihda za kumtafuta mmoja zinaendelea.

Alisema licha ya jeshi la Polisi kufanya doria katika machimbo hayo, changamoto kubwa iliyopo ni uhaba wa mawasiliano yanayochangia kwa kiasi kikubwa ucheleweshaji wa taarifa pindi kunapotokea tatizo.

Alitoa wito kwa wadau wa mawasiliano kupeleka mawasiliano ya uhakika katika eneo hilo linalokadiriwa kuwa na watu zaidi ya 5000.Reactions:

0 comments:

Post a Comment