Sunday, 11 June 2017

PROGRAMU YA KUKUZA UJUZI WA NGUVU KAZI YAZINDULIWA IRINGA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu(sera, bunge, kazi, vijana, na watu wenye ulemavu), Jenista Mhagama amezindua Programu ya kitaifa ya kukuza ujuzi wa nguvu kazi ya Taifa kwa vijana; mpango utakaowanufaisha vijana 3,400 katika kipindi cha mwaka 2017/2018.

Programu hiyo inayogharamiwa na serikali itatekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia taasisi ya Don Bosco Net Tanzania.

Akizindua program hiyo juzi katika viwanja vya chuo cha Don Bosco Iringa, Mhagama alisema serikali imeweka mipango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati ifikapo 2015.

“Mwelekeo wa miaka mitano ya sasa kuanzia 2016 hadi 2021 ni kujenga taifa la viwanda kwa kuzalisha bidhaa za kutosheleza mahitaji ya soko la nfani na kuuza nje ya nchi,” alisema.

Kwa umuhimu huo alisema serikali imeandaa program ya kitaifa ya kukuza ujuzi wa nguvu kazi ya Taifa ambayo utekelezaji wake umeanza kwa kutoa fursa kwa vijana kupata ujuzi katika sekta mbalimbali kama vile ya ushonaji nguo, utengenezaji bidhaa za ngozi, ujenzi, utalii, , teknolojia ya habari na mawasiliano, umeme, na ufundi wa magari, bomba na vyuma.

“Leo tunafanya uzinduzi wa stadi mbalimbali za kazi kwa vijana 3,440 watakaopata mafunzo kupitia vyuo nane vilivyopo chini ya taasisi ya Don Bosco Net Tanzania.

Alitaja mafunzo hayo na idadi ya vijana hao kuwa ni useremala (250), uashi (195), ufundi magari (302), uchongaji wa vipuri (158), ufundi bomba (195), ufundi vyuma (250), umeme (160), Tehama (1,010), kuweka terazo na vigae (120) na ushonaji nguo (800).

Alisema katika kuhakikisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016-2021) unatekelezwa ipasavyo, serikali kwa kupitia program hiyo ya kukuza ujuzi nchini inalenga kuwafikia vijana 100,000 watakaopata mafunzo kupitia program za uanagenzi.

“Lakini pia kutwakuwa na mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu 1,200,000, mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi 1,700,000 na kutambua na kurasimisha ujuzi uliopatikana kwa vijana 1,000,000 waajiriwa na waliojiajiri ili kuziba nakisi hiyo ya ujuzi,” alisema.

Kabla ya kutengeneza program ya kukuza ujuzi nchini, Mhagama alisema utafiti wa nguvukazi wa mwaka 2014 unaonesha asilimia 79.9 ya nguvu kazi iliyopo katika ajira ina kiwango cha chini cha ujuzi, asilimia 16.6 ina kiwango cha kati cha ujuzi na asilimia 3.6 tu ndiyo ina kiwango cha juu cha ujuzi.

Alisema ili nchi ifikie uchumi wa viwanda na kuwa ya kipato cha kati inahitaji asilimia 12 ya ujuzi wa kiwango cha juu, asilimia 34 ya kiwango cha kati na kutozidi asilimia 54 kwa ujuzi wa kiwango cha chini.

Uzinduzi huo umeshuhudiwa na Naibu waziri, Anthony Mavunde, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela, wabunge kutoka mkoa wa Iringa na Njombe na Mkuu wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco Africa Mashariki Fr. Simon Asira.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment