Friday, 2 June 2017

PESA ZA UCHAGUZI MKUU 2015, ZAWASIMAMISHA WATUMISHI SITA KYELA

Tokeo la picha la Hunter Mwakifuna

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya imewasimamisha kazi watumishi wake sita wanaotuhumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na pia fedha za makusanyo ya kakao za mwaka 2015.

Akitoa taarifa za kusimamishwa kazi kwa watumishi hao, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Dk Hunter Mwakifuna aliwataja waliosimamishwa kuwa ni Omary Mungi aliyekuwa Ofisa wa Uchaguzi, wahasibu Kassim Chakachaka na Omary Muya, Ofisa Usafirishaji Freedom Mwainunu, Ofisa Mipango na Mchumi Francis Mwaipopo.

Alisema Halmashauri pia imewaandikia barua waajiri wa watumishi wawili waliohamishwa ili taratibu za kuwachunguza zifanyike.

Aliwataja watumishi wanaokabiliwa na tuhuma hizo, lakini walihama kuwa ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ambaye alikuwa Msimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo la Kyela, Clemence Kasongo. Kwa sasa yuko Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya.

Mwingine ni aliyekuwa Mweka Hazina wa Wilaya, Alpha Baraza aliyehamishiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga.


Dk Mwakifuna alisema kusimamishwa kazi kwa watumishi hao kunatokana na agizo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani la kutaka kuwachunguza kutokana na tuhuma zinazowakabili za kutumia vibaya fedha za uchaguzi ambazo hazikubainishwa kiasi chake na pia, Sh milioni 31 za makusanyo yakakao.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment