Thursday, 15 June 2017

PEDESHEE NDAMA MTOTO YA NG'OMBE ARUDI URAIANI

Tokeo la picha la Pedeshee Ndama

Hatimaye mfanyabiashara Ndama Hussein maarufu ‘Pedeshee Ndama Mtoto ya Ng’ombe’ amelipa faini ya Sh200 milioni na kuepuka kifungo cha miaka mitano jela.

Faini hiyo iliyomuwezesha pia kupata dhamana, inatokana na shtaka la sita la kutakatisha Dola 540,000 za Marekani (Sh 1.2bilioni).

Kwa shtaka la kwanza hadi la tano ambayo yanaendelea kumkabili mahakamani, Ndama amekamilisha masharti ya dhamana aliyopewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mdhamini alisaini bondi ya Sh100 milioni, mshtakiwa mwenyewe aliwasilisha mahakamani hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Dola 270,200 (Sh600 milioni).

Kesi hiyo itatajwa Juni 16 ili kuangalia upelelezi wa shtaka la kwanza hadi la tano kama umekamilika au la.

Katika shtaka hilo, alikuwa akidaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 2014 jijini Dar es Salaam, akiwa mwenyekiti na mtia saini pekee wa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Limited na akaunti ya benki ya kampuni hiyo iliyoko kwenye Benki ya Stanbic, alijihusisha moja kwa moja kwenye uhamishaji wa Dola 540,000 na kuzitoa huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la uhalifu la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Ndama alilikubali shtaka hilo na kukana makosa mengine yakiwamo ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika mashtaka mengine yanayoendelea kumkabili, anadaiwa kuwa Februari 20, 2014 alighushi nyaraka ya kibali cha kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonyesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha maboksi manne ya dhahabu yenye kilogramu 207 na thamani ya Dola 8.28 milioni kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited wakati akijua si kweli.

Pia anadaiwa Machi 6, 2014 jijini Dar es Salaam, alighushi kwa kutengeneza hati ya kibali cha Umoja wa Mataifa, ofisi ya Dar es Salaam akijaribu kuonyesha kuwa kilo 207 za dhahabu kutoka nchini Congo zinazotarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited, zimesafirishwa bila jinai yoyote wakati akijua si kweli.

Pia anadaiwa Februari 20, 2014 alighushi fomu ya forodha yenye namba ya usajili R.28092 akionyesha kampuni ya Muru imeilipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dola 331,200 kama kodi ya uingizaji wa bidhaa ambazo zina uzito wa kilo 207 ambazo ni dhahabu yenye thamani ya Dola 8.28 milioni kutoka Congo.


 Shtaka jingine anadaiwa Februari 20, 2014, alighushi nyaraka ya bima kutoka Phoenix of Tanzania Assurance Company Ltd akionyesha kampuni ya Muru imeyawekea bima maboksi manne yaliyokuwa na dhahabu hiyo. Anadaiwa kati ya Februari 26 na Machi 3, 2014, Dar es Salaam kwa njia ya udanganyifu alijipatia kutoka kwa kampuni ya nchini Australia ya Trade TJL DTYL Limited Dola 540,000 baada ya kudanganya atawapa na kusafirisha dhahabu hizo

Reactions:

0 comments:

Post a Comment