Thursday, 29 June 2017

MNYIKA, MDEE, BULAYA WAFUNGUA KESI KUPINGA ADHABU ZA BUNGE

Image result for MDEE MNYIKA

Wabunge watatu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamefungua kesi ya kupinga adhabu waliyopewa na Bunge ya kutokuhudhuria vikao kutokana na kukiuka maadili na kanuni za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wabunge hao ambao ni Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Esta Bulaya, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika wamefungua kesi hiyo leo (Alhamisi) katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma ambayo imetajwa chini ya Jaji wa Mahakama Kuu, Hamisa Kalombola.

Katika kesi hiyo wabunge hao wamefungua kesi dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, Mwenyekiti wa kamati ya madaraka, Haki na Kinga za wabunge, Kapteni mstaafu George Mkuchika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika kesi hiyo namba 27 ya Mwaka 2017 wabunge hao waliwakilishwa na wakili wa kujitegemea, Fred Kalonga ambapo kwa upande wa Serikali uliwakilishwa na wakili wa Serikali, Angaza Mwipopo.

Katika kesi hiyo ya msingi, Myika anapinga adhabu iliyotolewa dhidi yake ya kutohudhuria vikao vya Bunge kwa siku saba na kudai kuwa hakuna mahali popote katika kanuni za Bunge kwenye adhabu ya aina hiyo.


Bulaya na Mdee wao wanapinga adhabu waliyopewa ya kutohudhuria vikao vya Bunge la saba, la nane na la tisa kinyume na kanuni na taratibu kwa kuwa hawakuitwa kwenye kamati kwa ajili ya kuhojiwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment