Thursday, 15 June 2017

MGODI WA DHAHABU IRINGA WAUA MMOJA
WIKI moja baada ya majambazi wenye silaha kuvamia machimbo mapya ya dhahabu ya Nyakivangala yaliyopo wilayani Iringa na kisha kujeruhi na kupora zaidi ya Sh Milioni 81, mtu mmoja ameripotiwa kufa baada ya kufukiwa na kifusi katika harakati za uchimbaji wa madini hayo.

Mtu huyo ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini aliyetajwa kwa jina la Vaspa Nyenza alifukiwa majira ya saa moja usiku wa Juni 11 katika moja ya mashimo ambayo uchimbaji wa madini hayo ulizuiwa kwasababu hakukuwa na nguzo na ngao kwa ajili ya usalama wa wachimbaji.

Nyenza alifukiwa katika shimo hilo akiwa na wenzake watatu waliookolewa wakiwa salama wakati wakijaribu kutafuta mchanga uliodhaniwa kuwa na madini hayo.

Akizungumza na wanahabari Mkuu wa Wilaya ya Iringa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Richard Kasesela alisema:

“Baada ya kufanikiwa kuwaokoa wachimbaji watatu, waokoaji hawakufanikiwa kumpata Nyenza kutokana na changamoto ya uokoaji iliyojitokeza.

Alisema udongo ulikuwa ukiendelea kudondoka kutoka kwenye miamba ya shimo hilo wakati jitihada za kuutafuta mwili huo zikiendelea.

“Juni 14 tulilazimika kuongeza nguvu kwa kujaribu kudhibiti udongo uliokuwa ukidondoka kutoka katika kuta za miamba ya shimo hilo na kufukua kifusi kilichomfukia marehemu huyo,” alisema.

Alisema mwili wa Nyenza uliokolewa kutoka katika shimo hilo majira ya saa 7.50 usiku wa kuamkia jana.

“Baada ya kutolewa mwili wa Nyenza ulisafirishwa hadi kijijini kwake Itengulinyi Kata ya Ifunda wilayani Iringa kwa ajili ya mazishi yaliyopangwa kufanyika jana,” alisema.

Akitoa pole kwa familia ya mrehemu, Kasesela aliwataka wachimbaji katika mgodi huo kuzingatia taratibu na kuchukua tahadhari muhimu ili kujinusuru na maafa vinginevyo serikali itaufunga mgodi huo.

Naye mmiliki wa mgodi huo, Thomas Masuka alisema atabeba gharama zote za uokoaji, usafirishaji na mazishi ya mchimbaji huyo mdogo kama taratibu zinavyowataka.

Wakati huo huo,  Jeshi la Polisi Mkoani Iringa limafanikiwa kuwakamata na kuwatia nguvu watu saba wanaotuhumiwa kushiriki katika tukio la kuvamia, kujeruhi na kupora kiasi kikubwa cha fedha kwa watu mbalimbali katika machimbo hayo.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi alisema;  “Mpaka sasa tayari tumefanikiwa kuwatia nguvuni watuhimiwa saba wakiwa na Bastola moja inayosadikika ilitumika katika uvamizi huo,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment