Thursday, 1 June 2017

MAWAKALA WA PEMBEJEO WALIOIDANGANYA SERIKALI WABAINIKA

Tokeo la picha la kassim majaliwa

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imebaini madudu katika uhakiki wa madeni ya mawakala wa mbolea kwa sababu baadhi yao hawakuwa waaminifu.

“Tulipoanzisha mfumo wa kutoa pembejeo kwa njia ya vocha kwa kuwatumia mawakala kupeleka pembejeo vijijini, tulibaini kuwa baadhi yao walikuwa siyo waaminifu. wakiorodhesha majina ya wakulima na kuandika kuwa wamewapa madawa na pembejeo wakati hawapo.”

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Juni mosi, 2017) wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Morogoro), Devotha Minja kwenye kipindi cha maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu bungeni mjini Dodoma.

Minja alitaka kujua ni kwa nini Serikali haijawalipa mawakala hao hadi sasa licha ya kuwa inatambua kwamba walifanya kazi ya kusambaza pembejeo hizo.

“Tulijikuta tuna deni la Sh 65 bilioni. Nilipokutana na mawakala wiki mbili zilizopita, niliwaahidi kwamba tutawalipa lakini ni lazima watupe muda tufanye uhakiki ili kubaini kama kweli pembejeo zilifika. Kati ya shilingi bilioni 35 za madeni ya awali, imebainika kuwa Sh 6bilioni tu ndiyo za halali. Bado kuna Sh30bilioni nyingine zinafanyiwa uhakiki,” amesema Waziri Mkuu.

 “Tumewasihi waendelee kuwa wavumilivu ili tukamilishe zoezi hili na tujue Serikali inadaiwa kiasi gani. Napenda niwahakikishie kuwa kazi hiyo inaendelea na tuko kwenye hatua za mwisho, na wale wote wenye madai halali ambao ni waaminifu watalipwa na Serikali.”

Amesema Akijibu swali la nyongeza ni kwa nini Serikali isiharakishe malipo hayo kwani kuna baadhi nyumba zao zimepigwa mnada na mabenki, na wengine wamepoteza maisha kwa sababu ya mshtuko.

Amesema wenye mabenki wameisikia kauli ya Serikali kwa hiyo hawana sababu ya kukimbilia kuuza mali za mawakala kwa njia ya mnada kwani hatua zinazochukuliwa na Serikali ni nzuri na zimeokoa mabilioni ya fedha.

Alisema watumishi wote wa umma waliohusika kwenye ubadhirifu huo, watachukuliwa hatua za kinidhamu.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment