Friday, 23 June 2017

MASENZA: MSIWAPE VIBALI VYA KULALA MISIKITINI WAGENI MSIOWAJUA

Image result for futari kilolo

MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amewaomba viongozi wa dini ya kiislamu kutowapokea wala kuwapa vibali vya kulala misikitini watu wasiowafahamu.

Aliyasema hayo juzi mjini Kilolo wakati mkuu wa wilaya hiyo, Asia Abdallah akiwafutisha waumini wa dini hiyo na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Akitoa agizo hilo Masenza aliwataka viongozi wa dini hiyo na wananchi kwa ujumla kutoa taarifa za wageni mbalimbali ambao uwepo wao katika maeneo yao unajenga mashaka.

“Upo ukarimu unaofanywa katika maeneo mbalimbali yenye misikiti, baadhi ya wageni wanaokosa sehemu za kulala kwasababu mbalimbali, uomba na kupewa nafasi ya kulala misikitini,” alisema.

Alisema sio kila anayetoa ombi hilo ana nia njema; kwani wapo wanaoweza kutumia fursa hiyo kufanya jambo lolote lenye madhara kwa jamii.

Akiwashukuru kwa kujitokeza kwa wingi katika Futari hiyo, DC Abdallah aliwataka wana Kilolo na watanzania kwa ujumla wao kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Dk John Magufuli za kupambana na kila aina ya uhalifu.

“Mwenyezi Mungu alipenda Dk Magufuli awe Rais wetu na kwa kweli kila mtu ameanza kuona matunda ya maamuzi ya watanzania yaliyofanywa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015,” alisema.

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amefanya mambo makubwa yanayoweza kushuhudiwa na vipofu na viziwi.

“Ni kwasababu kila anachofanya nafanya huku akiwa na hofu ya Mungu ndio maana anachukia maovu, anachukia ufisadi na anachukia wezi, tumuunge mkono,” alisema.

Awali Sheikh wa Mkoa wa Iringa, Abubakar Chalamila aliipongeza serikali ya mkoa wa Iringa akisema mwezi Mtukufu wa Ramadhani wa mwaka huu umechangia kuongeza mshikamano miongoni mwa wakazi wa mkoa wa Iringa.

“Mialiko hii ya Futari zinazoandaliwa na viongozi wa serikali, inakusanya watu wa dini zote na kurejesha upendo miongoni mwao,” alisema.

Katika kusaidia vita dhidi ya kuporomoka kwa maadili, Sheikh Chalamila aliwaomba viongozi wa serikali wawatumie mara kwa mara viongozi wa dini kwani kauli zao wakati fulani zinafika zaidi kuliko zile za viongozi wa siasa.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment