Saturday, 10 June 2017

MAJAMBAZI YAJERUHI, YAPORA MILIONI 81 MACHIMBO YA DHAHABU IRINGAWATU tisa wamejeruhiwa vibaya baada ya majambazi walio na silaha kuvamia machimbo mapya ya dhahabu yaliyopo katika kijiji cha Nyakivangala, Isimani wilayani Iringa mkoani Iringa na kupora zaidi ya Sh Milioni 81 taslimu.

Pamoja na kiasi hicho cha fedha, majambazi hao wanadaiwa kupora dhahabu zaidi ya gramu 400, simu nne za mkononi na baadhi ya mali za wafanyabiashara katika eneo hilo linalokimbiliwa na wachimbaji na wachuuzi wa biashara mbalimbali.

Akizungumza na wanahabari jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema tukio hilo linalodaiwa kudumu kwa zaidi ya saa moja lililitokea majira ya saa nne usiku juzi.

Kasesela ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa alisema majambazi hao ambao idadi yao haikufahamika walifanikiwa kukimbia muda mfupi kabla askari Polisi kufika katika eneo hilo lililopo zaidi ya kilometa 50 kutoka Iringa Mjini.

“Majambazi hao wanaodaiwa kutumia gari aina ya Landcruiser na nyingine ndogo ambazo kwa pamoja hazikuweza kujulikana umiliki na namba zake,” alisema.

“Baada ya kuvamia walifyatua risasi ovyoovyo, wakawapiga na kuwajeruhi baadhi ya watu na kupora kiasi hicho cha fedha na kutokomea,” alisema.

Kasesela alisema taarifa za awali zinaonesha majambazi hao walikuwa wakimfuatilia mmoja wa wafanyabiashara wa madini hayo aliyekuwa na kiasi kikubwa cha fedha katika machimbo hayo.

Alimtaja mfanyabiashara huyo kuwa ni Mginya Paulo Dadaye (38) mkazi wa Morogoro aliyeporwa zaidi ya Sh Milioni 79 baada ya kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwa ni pamoja na mikononi na miguuni.

“Walikuwa wakimsaka mfanyabiashara huyo kwa kuwauliza, kuwapiga na kuwapora wafanyabiashara wengine mpaka walipofanikiwa kumkamata, kumjeruhi na kumpora,” alisema.

Aliwataja wengine waliojeruhiwa katika tukio hilo kuwa ni pamoja na Bakari Beka, Sungari Shija (24) mkazi wa Geita, Fadhili Nalinga mkazi wa Morogoro, Nsurwa Msanga (30) mkazi wa Bariadi na Odrick Michael (33) mkazi wa Ipogolo Iringa.

Wengine ni Kitandu Mabula (27) mkazi wa Tanga, Danie Masegu (40) mkazi wa Simiyu na Elia Mushi (26) mkazi wa Moshi ambao wote wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa.

Alitoa wito kwa wachaimbaji na wafanyabiashara wa madini katika eneo hilo kutotembea na kiasi kikubwa cha fedha na kufanya biashara hiyo kwa kutumia mitandao ya simu au huduma za kibenki zilizoko Iringa Mjini.


Jeshi la Polisi Mkoani Iringa limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na linaendelea na msako wa majambazi hao.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment