Sunday, 18 June 2017

LIPULI FC YAZINDUKA


KLABU ya soka ya Lipuli ya mjini Iringa imezinduka kutoka kwenye migogoro ya uongozi isiyokwisha kwa kutangaza kuanza maandalizi kamambe yatakayoiwezesha timu hiyo kushiriki vyema Ligi Kuu, msimu ujao.

Wakizungumza na wanahabari juzi, viongozi hao walitangaza kuitishwa mzigo wa kutafuta fedha za maandalizi hayo yaliyoanza juzi, kamati yake ya Mipango na Fedha inayoongozwa na July Sawani.

Katibu wa Lupili FC, Willy Chikweo alisema wameamua kuyapa kisogo majungu na migogoro yote inayikabili timu hiyo ili waanze maandalizi yatakayowasaidia kubaki katika ligi hiyo waliyoisotea kwa miaka 17.

“Napenda kuwatangazi wapenzi wa soka wa mkoa wa Iringa na Tanzania kwa ujumla kwamba tumekabidhi masuala yote yanayohusu utafutaji wa fedha kwa kamati hii ya Mipango na Fedha,” alisema.

Alisema matumizi ya fedha hizo zikiwemo zile watakazopata kutoka kwa wadhamini yataratibiwa na uongozi wa Lipuli FC kwa kushirikiana na kamati hiyo ili kuongeza uwazi yake.

“Hakuna fedha itakayotumika nje ya shughuli zinazohusu klabu hii. Naomba wadau wote muiamini kamati hii kama mlivyoiamini katika mchakato uliowezesha timu hii kupanda daraja,” alisema.

Chikweo aliwataja wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni Jully Sawani ambaye ni Mwenyekiti, Shabani Lushino Katibu, Emanuel Mpangala Makamu Mwenyekiti, Shadrack Masanika Mweka Hazina na wajumbe ni Husna Mtasiwa, Luka Kambanyuma, Jully Mbawala na Jully Mgonja.

Kwa pande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo, alisema kamati yake imepokea kwa mikono miwili jukumu la kusaidia Lipuli FC kufikia malengo yake katika ligi hiyo.

“Kamati hiyo iko tayari kuanza kazi bila kupoteza muda zaidi, tunajua muda umetutupa mkono; tunaomba makampuni mbalimbali ya mkoani hapa yajitokeze kwa wingi kuidhamini timu hii,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa kamati hiyo alisema watajitahidi kuwafikia wadau mbalimbali wa ndani na nje ya mkoa wa Iringa ili waiwezeshe timu yao kushiriki vyema ligi hiyo.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment