Friday, 23 June 2017

LIPULI FC YAPELEKWA MAHAKAMANI

Image result for Lipuli FC

HABARI za uhakika kutoka katika uwanja wa haki wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa zimeuthibitishi mtandao huu kwamba mmoja wa wanachama wa Klabu ya Lipuli FC ya mjini Iringa amefungua kesi kupinga baadhi ya mambo yanayoendelea katika klabu hiyo.

Lipuli FC inatarajia kushiriki Ligi Kuu msimu ujao ikiwa ni miaka 17 tangu ishuke daraja.

Wakiwa na kiu kubwa ya kuona Ligi hiyo wadau wa mchezo huo wa ndani na nje ya mkoa wa Iringa walijitokeza kwa hali na mali kusaidia harakati za kuipandisha timu hiyo.

Harakati hizo ziliratibiwa na kamati ya mipango na fedha ya klabu hiyo kwa kushirikiana na kamati ya utendaji ambayo hivikaribuni ilalamikiwa na wapenzi na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo kung’ang’ania madaraka.

Akizungumza na mtandao huu, mmoja wa maafisa wa mahakama hiyo (jina linahifadhiwa) alisema mwanachama huyo (hakutajwa jina) alifungua kesi hiyo jana kupitia kwa wakili wake aliyetajwa kwa Musa Mhagama.

“Kesi imeshafunguliwa, wakati wowote baada ya siku kuu ya Idd, wahusika watapewa samansi za kuitwa mahakamani,” alisema.

Alisema katika shauri hilo, mwanachama huyo ameishitaki klabu ya Lipuli FC kama mshtakiwa wa kwanza, Chama cha Mpira wa Miguu Manispaa ya Iringa mshtakiwa wa pili na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama mshitakiwa wa tatu.

Baada ya kusoma taarifa hiyo kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, Mwenyekiti wa Lipuli FC Abou Changawa maarufu kwa jina la Majeki alisema; “wacha waendelee na kesi sisi tunaendelea kutengeneza timu, hatuna wasiwasi wowote watashindwa kama walivyoshindwa siku za nyuma. Kila siku nasema kuna watu wanajifanya Lipuli wakati sio Lipuli nawaonea huruma na hao wanaowafadhili.”

Reactions:

0 comments:

Post a Comment