Wednesday, 21 June 2017

KASESELA AWATAKA WAMILIKI WA MAJENGO IRINGA KULIPA KODI

Image result for Kasesela

MKUU wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela amewataka wamiliki wa majengo wilayani kwake kuzitumia siku tisa zilizobaki kulipa kodi ya majengo ili waondokane na usumbufu wa kosa la ukwepaji wa kodi hiyo.

Zikiwa zimebaki siku hizo, taarifa iliyotolewa na Afisa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Iringa, Ernest Kagali inaonesha asilimia 41 tu ya wamiliki wa majengo wilayani Iringa wamelipa kodi hiyo hadi wiki iliyopita.

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake jana, Kasesela alisema kodi hizo zinakusanywa kwa kutimia taarifa za walipa kodi zilizokabidhiwa kutoka kwa serikali za mitaa.

“Awali kodi hizo zilikuwa zikikusanywa na serikali za mitaa lakini kuanzia Julai mwaka jana TRA ilipewa jukumu la kutathimini, kukadiria na kukusanya kodi za majengo,” alisema.

Alisema “kodi hizo ni ndogo, tumieni muda uliobaki kuzilipa ili mkwepe faini na usumbufu mwingine utakaojitokeza baada ya zoezi la kukusanya kodi hizo kwa mwaka wa fedha uliopita kufungwa Juni 30, mwaka huu.”

Akitoa ufafanuzi wa malipo ya kodi hizo, Kagali alisema zinalipwa kwa kupitia benki mbalimbali zinazofanya kazi na TRA baada ya kujaza fomu maalumu inayotolewa na TRA.


“Tumeshatoa notisi kwa wamiliki wote ambao taarifa zao zilikuwepo kwenye ofisi za serikali za mitaa, kama hawajapata, pamoja na wale ambao taarifa zao hazipo wafike ofisi za TRA ili wakamilishe taratibu za kufanya malipo hayo,” alisema.

Alisema wamiliki wa majengo watakaoshindwa au kukaidi kulipa kodi hiyo kwa wakati, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini au mali kutaifishwa.

 “Wale ambao hawatalipa kodi hiyo watatozwa faini kila mwezi na wakiendelea kulimbikiza faini, tutawafikisha mahakamani kwa kutumia Sheria ya Kodi ya Mamlaka ya Miji, Sura 289,” alisema.

Ikitokea wakaendelea kutokulipa alisema Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 itaamua ambapo TRA itakamata mali zao na kuziuza ili kufidia thamani ya tozo wanalopaswa kulipa.

Alisema TRA inakusanya kodi ya majengo baada ya kufanyika kwa mabadiliko ya sheria tatu zilizo chini ya Sheria za Fedha ya mwaka 2016.

Sheria hizo ni; Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, sura ya 290; Sheria ya Kodi ya Mamlaka ya Miji, sura ya 289 na Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA), sura ya 399.


Alisema ulipaji kodi kila mwaka hautawagusa wamiliki wa nyumba za ibada (zisizo za biashara), walemavu na wazee wa miaka 60 watakaotambuliwa kwa kuzingatia taratibu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment