Thursday, 1 June 2017

BAJETI YA NISHATI NA MADINI KUSOMWA BILA MUHONGO LEO

Tokeo la picha la profesa muhongo

MAKADIRIO ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 yanatarajiwa kuwasilishwa bungeni leo huku ikiwa haina waziri.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah pamoja na kwamba hakuthibitisha waziri anayesoma leo bajeti hiyo, alisema taarifa alizokuwa nazo awali zilionesha mwenye dhamana ya wizara hiyo ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.

Bajeti hiyo ambayo ni ya mwisho baada ya wizara zote kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi yake bungeni, ilitarajiwa kuwasilishwa tangu wiki moja iliyopita lakini iliahirishwa kutokana na sababu mbalimbali.

Mara ya kwanza iliahirishwa baada ya aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo kupata matatizo ya kifamilia (alifiwa na dada yake), lakini hata baada ya kusogezwa mbele ilishindikana kusomwa baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa waziri huyo.

Profesa Muhongo alitenguliwa uteuzi wake baada ya Dk Magufuli kupokea ripoti ya uchunguzi wa makanikia iliyowasilisha Mwenyekiti wake, Profesa Abdulkarim Mruma ambaye iliibua madudu mengi likiwemo la kuibiwa kwa makinikia hayo.

Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, bajeti hiyo inatakiwa iwasilishwe na waziri kamili na wanaotajwa kuweza kuwasilisha bajeti hiyo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachene na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi.

Mwingine ni Mwijage. Simbachawene aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini katika Serikali ya Awamu ya Nne.


Kwa sasa wizara hiyo iko chini ya Naibu Waziri ambaye ni Dk Medard Kalemani. Alipotengua uteuzi wa Profesa Muhongo, Rais Magufuli alisema nafasi yake itajazwa baadaye. Awali, Jenista alipoulizwa kuhusu anayehusika kusoma bajeti hiyo, alisema tayari amewasilisha barua katika Ofisi ya Katibu wa Bunge bila kutaja jina ni la waziri gani.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment