Sunday, 25 June 2017

ASKOFU MDEGELA AIPONGEZA CCM KWA KUJIREKEBISHA
ASKOFU Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dk Owdenburg Mdegela ameipongeza serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa hatua mbalimbali inazochukua kujirekebisha.

Dk Mdegela aliyasema hayo jana alipoungana na mamia ya wakazi wa mkoa wa Iringa waliofanya maandamano ya amani mjini Iringa kupongeza juhudi zzinazofanywa na Rais Dk John Magufuli katika kushughulikia changamoto zinazolikabili Taifa.

Maandamano hayo yaliyopokolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza yakitokea bustani ya manispaa ya Iringa hadi uwanja wa Mwembetogwa yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, siasa na serikali, watumishi, wanafunzi, wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo toka wilaya zote za mkoa wa Iringa.

Alisema moja ya kosa kubwa lililofanywa na serikali lilikuwa ni kuua Azimio la Arusha la mwaka 1967.

“Hatukupaswa kuua Azimio la Arusha pamoja na kwamba kuna mambo yalipaswa kubadilishwa. Kimsingi azimio lile lilikuwa na mambo mengi ya msingi ambayo ni ya faida kwa Taifa, hayo ni pamoja na maadili kwa viongozi na msingi wa kujitegemea,” alisema.

Alisema serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ilichoka; lakini kwa kupitia Rais Magufuli imeanza kujirekebisha ikiwa ni pamoja na kutembea katika misingi ya Azimio la Arusha, hatua inayopaswa kupongezwa hadharani.

“Anayempinga Rais anayekamata wezi, watumishi hewa na anayepambana kulinda rasilimali za nchi kwa manufaa ya watanzania wote na kuhimiza uwajibikaji lazima atakuwa alipata matokeo mabayo ya mtihani wa darasa la saba na kidato cha nne,” alisema.

Alipongeza maandamano hayo yaliyoandaliwa na wazee na wadau wengine wa mkoa wa Iringa akisema yanamtia moyo rais kuendeleza mapambano aliyoyaanzisha.

“Tunapaswa kuiona falsafa ya kiongozi wetu pamoja na kwamba wapo watu wanambeza kwa maneno mengi ya kuudhi lakini wanaombeza Magufuli wakumbuke kwamba hata Mungu alibezwa na theluthi moja ya malaika zake,” alisema.

Dk Mdegella alisema mkoa wa Iringa umebarikiwa kwa kuwa na vyanzo vingi vya maji, rasilimali misitu na ardhi yenye rutuba ambavyo kwa pamoja vinaweza kutumiwa kuunga mkono azma ya Rais ya kuwa na nchi yenye viwanda.

“Kwa kutumia rasilimali hizo tunaweza kuifanya Iringa kuwa mkoa wenye viwanda vingi vya kusindika samaki, kutengeneza bidhaa mbalimbali za mbao na vya usindikaji wa matunda na vyakula,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania, Stanslaus Mhongole alisema wananchi wa mkoa wa Iringa wana kiu kubwa ya kuona baadhi ya viwanda vilivyokufa baada ya utawala wa Mwalimu Nyerere, kikiwemo kiwanda cha Coca cola vinafufuliwa.


Akipokea maandamano hayo Mkuu wa Iringa alisema katika utangulizi wake Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 inasema katika miaka mitano ijayo, CCM ikiwa madarakani itazielekeza serikali zake kutumia nguvu zake zote kuondoa umasikini, kutatua tatizo la ajira hasa kwa vijana, katika vita dhidi ya rushwa na ubadhilifu wa mali za umma na kudumisha amani, ulinzi na usalama.


Maandamano hayo yalihitimishwa kwa wahadhili wa vyuo vikuu vinne vya mjini Iringa kutoa mada juu ya vita ya uchumi iliyofanywa na viongozi wa awamu zote nne zilizopita hadi mwanzo wa awamu hii ya tano.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment