Sunday, 14 May 2017

WAVUNAJI WA MITI SAO HILL, WATAKA MIKATABA YA HADI MIAKA MITANO
UMOJA wa Wavunaji Miti katika Shamba la Saohil (UWASA) wameiomba serikali iwape mikataba ya uvunaji ya hadi miaka mitano kwa mkupuo ili wawe na uhakika wa malighafi hiyo katika juhudi zao za kutimiza matakwa ya serikali ya awamu ya tano kwenye sera ya viwanda.

Pamoja na ombi hilo wameiomba serikali ifanye marekebisho ya sheria, kanuni na taratibu mbalimbali za biashara ya mazao yatokanayo na miti waliyodai yanazidi kuporomoka bei; ili zikidhi matakwa ya sasa na kuongeza tija.

Walitoa maombi hayo kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamuhuri William katika mkutano wao uliofanyika katika ukumbi wa shamba hilo juzi, mjini Mafinga kujadili changamoto mbalimbali zinazowagusa wavunaji hasa wadogo.

Katibu wa umoja huo, Dk Basil Tweve alisema licha ya wengi wao kuwa na mitaji, wavunaji wadogo wanashindwa kufanya maamuzi magumu ya kuingia kwenye teknolojia ya viwanda kwa kuwa hawana uhakika wa kupata malighafi hiyo.

“Miaka miwili iliyopita ugawaji wa malighafi hiyo ulifanywa kwa kujaza fomu, wako waliopata na wako waliokosa. Fomu hizo huanza kutolewa mwezi Januari, lakini mwaka huu ni kizungumkuti kwani fomu hizo hazijatolewa hadi sasa,” alisema.

Kuhusu kuporomoka kwa bei, Dk Tweve alisema mwaka 2015/2016 mbao kutoka katika magogo yenye ujazo wa mita ya mraba moja ziliuzwa kwa kati ya Sh 480,000 na Sh 500,000 lakini mwaka 2016/2017 zinauzwa kwa Sh 350,000.

“Bei imeshuka kutokana na hali halisi ya soko na kutokuwepo kwa bei elekezi ya mazao ya misitu. Wakati mabadiliko hayo yakitokea bei ya kununua magogo na kodi zake mbalimbali zinazidi kupanda,” alisema.

Akizungumzia kanuni na taratibu mbalimbali za uendeshaji wa biashara hiyo kisheria, mmoja wa wanachama wa UWASA, Godfrey Mosha alisema zipo zinazotakiwa kufanyiwa marekebisho na zinazotakiwa kuondolewa kwa kuwa zimekuwa mzigo kwa wadau.

Alizitaja zinazotakiwa kuondolewa kuwa ni pamoja na ada ya ukusanyaji wa mbegu za miti kwa kuwa ni kikwazo na utunzaji wa mazingira, hati ya kusafirishia mbao au magogo, faini ya kuchelewa kutoa magogo shambani na tozo kwa ajili ya kutega maji eneo la msitu kwenda kwa wananchi.

Zinazotakiwa kufanyiwa marekebisho ni pamoja na gharama za usafirishaji wa mbao au magogo nje ya nchi, siku 30 za uvunaji ziongezwe, tozo za usafirishaji mbao na magogo barabarani na wavunaji wenye viwanda wapewe mikataba ya miaka mitano ili wasiombe kila mwaka.

Akiahidi kuyafikisha maombi yanayotakiwa kufikishwa kwa Mkurugenzi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mkuu wa Wilaya alisema serikali inatambua mchango wa maendeleo unaotolewa na wavunaji hao.

Naye Meneja wa Shamba la Saohill, Saleh Beleko alipokea maoni ya kanuni, sheria na taratibu mbalimbali zinazoongoza shughuli hiyo ya uzalishaji na uuzaji wa miti akisema atayafikisha wizarani ili yafanyiwe kazi.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment