Thursday, 18 May 2017

SERIKALI YARIDHISHWA UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA YA KILOLOUJENZI wa hospitali ya wilaya ya Kilolo mkoani Iringa unatarajia kutumia kiasi cha Sh Bilioni 12 mpaka kukamilika kwake.

Kukamilika kwa hospitali hiyo kumeelezwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Selemani Jafo kutarahisisha upatikanaji na utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Baada ya kuanzishwa kwake mwaka 2002, kutoka katika wilaya ya Iringa, wilaya ya Kilolo imekuwa ikitoa huduma za hadhi ya hospitali kupitia hospitali teule ya wilaya ya Ilula inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa.

Akizungumza na viongozi na watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo katika ziara yake aliyofanya Jumanne, Jafo alisema analidhishwa na usimamizii na kasi ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Aliwaahidi viongozi wa halmashauri hiyo kwamba serikali itaendelea kutoa fedha kwa kadri inavyowezekana ili ujenzi wa hospitali hiyo ukamilike mapema.

“Kazi mnayofanya ni  nzuri  sana, nimefarijika na nitaendelea kumshauri Mheshimiwa  Rais ili pesa zaidi ziletwe wilayani Kilolo kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa hospitali hii,” alisema.

Hata hivyo alisema kabla serikali haijaleta fedha zingine, kama inavyotakiwa, halmashauri hiyo italazimika kuwasilisha taarifa ya matumizi ya fedha zilizopita ili waweze kuomba na kupewa fedha zingine kwa ajili ya ujenzi huo.

Wakati huo huo, Waziri Jafo serikali imetoa Sh Milioni 239 kwa ajili ya ujenzi wa daraja katika mto Kiwalamo wilayani humo.

“Namuagiza mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanasimamia vyema ujenzi wa daraja hilo, lijengwe kwa kuzingatia thamani ya fedha zilizotolewa ili kuondoa kabisa changamoto waliyokuwa wanapata wananchi waliokuwa wanavuka pande mbili za mto huo,” alisema.

Kuhusu barabara ya kiwango cha lami kutoka Iringa Mjini hadi makao makuu ya wilaya hiyo, Kilolo, Jafo alisema kwa kuwa suala lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya 2015-2020 wananchi wanapaswa kuwa wavumilivu kwani itafanyiwa kazi.


Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamotto aliipongeza serikali ya awamu ya tano kwa hatua zote inazochukua kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo lake la Kilolo akisema zinagusa maisha yao ya kila siku.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment