Tuesday, 30 May 2017

PAMOJA NA KILIO CHA MASHABIKI, WENGER APEWA MKATABA WA MIAKA MIWILI ARSENAL

Tokeo la picha la arsene wenger

Kocha Mkuu wa klabu Arsenal Arsene Wenger amekubali kuchukua mkataba wa miaka miwili katika klabu hiyo, uamuzi utakaomfanya awe amekaa klabuni hapo kwa miaka 23.

Mpaka sasa Mfaransa huyo ana miaka 21 katika klabu hiyo ambayo mashabiki wake wanachukizwa na ukame wa vikombe, hasa cha ligi kuu.

Wenger na mmiliki wa klabu hiyo Stan Kroenke walikutana Jumatatu kuamua hatima ya meneja huyo, na kisha uamuzi wao uliwasilishwa kwenye mkutano wa bodi uliofanyika leo Jumanne. Arsenal wanapanga kutangaza rasmi uamuzi huo Jumatano.

Msimu wa 2016/2017 Gunners walimaliza Ligi ya Premia wakiwa nafasi ya tano, mara yao ya kwanza kumaliza chini ya nafasi ya nne tangu Wenger alipojiunga nao mwaka 1996.

Walimaliza alama 18 nyuma ya mabingwa Chelsea, lakini walifanikiwa kuwachapa Blues katika fainali ya Kombe la FA uwanjani Wembley Jumamosi.

Mkataba wa Wenger ulikuwa unamalizika mwishoni mwa msimu huu.
Wenger aliongoza Gunners kushinda mataji matatu ya Ligi ya Premia na pia vikombe vinne vya FA misimu yake tisa ya kwanza kwenye usukani.
Mwaka 2003-04, aliibuka meneja wa kwanza tangu 1888-89 kuongoza timu iliyomaliza ligi kuu bila kushindwa.

Lakini baada ya kushinda Kombe la FA mwaka 2005, walisubiri kwa miaka mingine tisa – sawa na siku 3,283, kabla ya kushinda kikombe kingine.
Walilaza Hull City fainali ya Kombe la FA mwaka 2014 na kisha wakashinda kikombe hicho tena mwaka uliofuata.

Baadhi ya mashabiki wa Arsenal wamekuwa wakimtaka Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 67 ajiuzulu, hasa baada ya matokeo mabaya msimu huu. Shutuma zaidi zilitolewa waliposhindwa kwa jumla ya mabao 10-2 na Bayern Munich katika hatua ya 16 bora Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mwezi Machi.

Walimaliza msimu wakiwa wameshinda mechi tano mfululizo, lakini matokeo hayo hayakutosha kuwawezesha kuwapita Liverpool waliomaliza nafasi ya nne na kujaza nafasi ya mwisho ya kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Jumamosi, Wenger aliambia BBC kwamba shutuma na uokosoaji aliokumbana nao msimu huu ni wa “kufedhehesha” na kwamba hatawahi kuusahau kamwe maishani.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment