Sunday, 14 May 2017

NYANDA ZA JUU KUSINI WATOA MAONI MABORESHO YA SERA YA UTALII


WADAU wa sekta ya utalii wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wamesema Sera ya Utalii ya mwaka 1999 imepitwa na wakati na inahitaji maboresho makubwa ili iendane na mabadiliko ya kiteknolojia, kijamii, kiuchumi, kisiasa na mazingira yanayoendelea kutokea duniani.

Wadau hao walikutana mjini Iringa juzi kwa uratibu wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) inayofanya kazi na Wizara ya Maliasili na Utalii ya kukusanya maoni ya wadau ya uhuishwaji wa sera hiyo.

Wakitaja vivutio mbalimbali vya utalii vilivyoko katika wilaya mbalimbali za mikoa yao, wadau hao walisema sera iliyopo imeviweka kanda vivutio vilivyoko nje ya hifadhi za Taifa pamoja na kwamba vina mchango mkubwa kwa maendeleo ya sekta hiyo na Taifa kwa ujumla.

“Kwa mantiki hiyo ni muhimu kurekebisha sera ya Utalii iliyopo ili iendane na taratibu, mipango na mitazamo ya kitaifa, kikanda na kimataifa ikiwemo itifaki, mikataba na makubaliano yanayohusu utalii,” alisema Profesa Raphael Mwalyosi anayeiwakilisha ESRF katika mchakato huo.

Prof Mwalyosi alisema ingawa sera iliyopo kulenga utalii unaokuza uchumi na kupunguza umasikini wa watanzania kwa kuzingatia utalii endelevu, rasilimali za utalii zinaendelea kutumika bila ya kuwa na faida ya moja kwa moja kwa wananchi.

Alisema pamoja na kwamba hakujawa na msukumo wa dhati wa kukuza utalii wa ndani na utamaduni, kupanua wigo wa rasilimali za utalii na maeneo ya utalii; njia zinazotumika kutangaza utalii nje ya nchi zina gharama kubwa na kuufanya usiwe endelevu.

“Wakati utalii sasa unaanza kuelekezwa katika maeneo yaliyo nje ya hifadhi ambako Wizara ya Maliasili na Utalii haina mamlaka ya moja kwa moja ya kiusimamizi katika utekelezaji wa sera ya utalii na hivyo kuchangia uharibifu wa mazingira na rasilimali zake bila kuwa na matokeo chanya kwa sekta,” alisema.

Awali Mkurugenzi wa Idara ya Utalii nchini, Zahoro Kimwanga alisema uhishwaji wa sera hiyo utazingatia namna ambavyo wazawa wataweza kuwa wanufaika namba moja kwa kuwaandalia mazingira rafiki ya kuendesha biashara ya utalii.

“Tunataka kuibadilisha sera hiyo ili iweze kujibu changamoto za aina ya utalii wa sasa ambao kipindi cha nyuma haukuwepo,” alisema na kutolea mfano wa utalii wa kiutamaduni unaoendelea kukua kwa kasi kubwa.

Kutokana na hali hiyo, Kimwanga alisema marekebisho ya sera hiyo inahitaji mchango mkubwa kutoka kwa wadau kwa kuwa sekta ya utalii inaendeshwa kwa kiasi kikubwa na sekta binafsi katika utoaji wa huduma na biashara za utalii.

Alisema utalii ni sekta yenye mchango mkubwa katika kuongeza pato la Taifa ukichangia zaidi ya asilimia 17 na ukitoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zaidi ya Milioni 1.5.

Alisema sekta hiyo inayoshika nafasi ya pili nchini kwa kuvutia wawekezaji imeshika nafasi ya kwanza katika kuliingizaTaifa fedha za kigeni kwa miaka minne mfululizo kati ya mwaka 2012 na 2015.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment