Sunday, 14 May 2017

MWENYEKITI WA KIJIJI IKUNGI AVULIWA MADARAKA

MJ5

MKUTANO maalum wa Kijiji cha Ikungi wilayani Ikungi mkoani Singida umemuondoa Mwenyekiti wa kijiji hicho Hussein  Ikusi kutokana na matumizi  mabaya ya madaraka kwa kufanya ubadhirifu wa mali za kijiji zenye thamani ya shilingi milioni 9.

Ubadhirifu huo aliufanya  toka alipoingia madarakani mwaka  2014 akishirikiana na aliyekuwa mtendaji wa kijiji hicho Hamis  Isango aliyehamishiwa kijiji cha Irisya.

Hayo  yalibainika baada ya halmashauri ya kijiji kuitisha kikao maalum tarehe 24 aprili mwaka 2017 wakimtuhumu mwenyekiti kwa hoja zipatazo 5.

Hoja hizo ni kushindwa kusimamia mali za kijiji,kushindwa kusimamia mipaka ya kijiji,kushindwa kuonyesha ushirikiano na uongozi wa halmashauri ya wilaya,Ofisi ya mkuu wa wilaya na taasisi za serikali zilizopo wilayani,kuwa chanzo cha migogoro badala ya kuwa mtatuzi na kushindwa kusimamia usomaji wa mapato na matumizi ya kijiji kwa mujibu wa sheria kwa kipindi cha  miaka miwili na nusu.

Ubadhirifu huo umebainishwa na mkaguzi wa mahesabu ya ndani Kitundu Mkumbo aliyeagizwa na mkuu wa wilaya hiyo Miraji Mtaturu kufanya ukaguzi wa mapato na matumizi ya kijiji baada ya kupokea tuhuma kuhusiana na mwenyekiti huyo.Reactions:

0 comments:

Post a Comment