Tuesday, 30 May 2017

BABA AKATA MAKALIO YA MWANAE


Mwanamume mmoja Mkazi wa Ndofe, Wilayani Nyamagana Mkoani Mwanza amemfanyia kitendo cha ukatili mtoto wake kwa kumkata na kisu sehemu za makalio kwa madai ya utoro shuleni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Ahmed Msangi amemtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Nuhu James (50) anayedaiwa kumfanyia ukatili mtoto Ndalo Nuhu (14) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Igoma kwa kumfunga kamba miguuni na mikononi kisha kumchapa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na baadaye kumkata na kisu sehemu za makalio.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa aliaamua kumfanyia ukatili wa aina hiyo mtoto wake baada ya kugundua kwamba mwanaye ni mtoro shuleni.

Kamanda Msangi amesema baada ya mama wa mtoto alipoona ukatili anaofanyiwa mwanaye na hali yake kiafya kuzidi kubadilika alishindwa kuvumilia na kuamua kutoa taarifa kituo cha polisi.


Kamanda Msangi amesema kuwa polisi wapo katika upelelezi na mahojiano na mtuhumiwa pindi uchunguzi utakapokamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani huku majeruhi akipelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu na hali yake inaendelea vizuri.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment