Tuesday, 30 May 2017

ASKARI WA TANAPA WATAKA KUJUA LUGHA ZA KIMATAIFA KUBORESHA UTALII
ASKARI wa hifadhi za Taifa wanaohitimu mafunzo ya uongozaji watalii kwa miguu kupitia program inayoratibiwa na Mradi wa Kuimarisha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST) wameomba kufundishwa lugha mbalimbali za kimataifa ili kuboresha huduma hiyo.

Awamu ya tatu ya mafunzo hayo yaliyohusisha askari 24 kutoka katika hifadhi za Taifa 16 nchini yalihitimishwa jana katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha, yalikofanyika pia mafunzo ya awamu ya kwanza na ya pili yaliyojumuisha askari 40.

Pamoja na kufundishwa jinsi ya kuwaongoza watalii kufanya utalii wa kutembea kwa miguu hifadhini, askari hao hufundishwa namna ya kuwaepusha watalii na hatari ya wanyama wakali, kujua tabia za wanyama, kupita vichakani, namna ya kutoa huduma ya kwanza na matumizi ya silaha.

Katika risala yao iliyosomwa na Tumaini Magesa wa Hifadhi ya Taifa ya Sadani, wahitimu hao 24 walisema utalii wa kutembea kwa miguu utavutia zaidi ikiwa watawezeshwa kumudu kuzungumza kwa ufasaha lugha mbalimbali za kimataifa kama kingereza, kifaransa na kijerumani.

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Ethan Kinsey alikiri ufahamu wa lugha za kimataifa kuwa ni changamoto kubwa kwa washiriki wa mafunzo hayo akisema hiyo ni kutokana na mafunzo hayo kutolewa kwa muda mfupi.

Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’ataki alisema: “waongoza watalii wanatakiwa kuwa wazuri kwenye lugha za kimataifa, kwa kuanzia jitihada zinatakiwa kuelekezwa kwenye lugha ya kingereza na matumizi ya fursa zilizopo kujifunza lugha zingine za kimataifa.”

Kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF), alisema SPANEST inatoa mafunzo kwa askari hao ili kusaidia kuboresha shughuli za uhifadhi na utalii katika hifadhi mbalimbali nchini.

Akifunga mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku 30, Kaimu Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA), Mtango Mtahiko alisema mafunzo kwa askari wao yanatolewa kwa kuzingatia mabadiliko yanayotokea mara kwa mara katika sekta hiyo ya uhifadhi na utalii.

Alisema mafunzo hayo yanatolewa kupitia mikakati ya TANAPA kwa kushirikiana na wadau wake inayolenga kunyanyua huduma ya utalii na uhifadhi nchini.

Alisema utalii wa kutembea kwa miguu unamfanya mtalii awe jirani na mazingira, mimea na wanyama na kufahamu sifa na tabia zake; ukiboreshwa utavutia watalii wengi zaidi na hivyo kuliongezea taifa mapato.

Mtahiko alisema utalii wa kutembea kwa miguu ni aina ya utalii inayokua kwa kasi kubwa hivyo ni fursa tosha inayoweza kuchangia kukuza sekta ya utalii nchini kama uwezekezaji wake utakuwa wa kutosha.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment