Monday, 10 April 2017

SERIKALI YAUNDA KIKOSI KAZI KUNUSURU BONDE LA MTO RUAHA MKUU

Tokeo la picha la Januari Makamba


TAMKO LA WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS - MUUNGANO NA MAZINGIRA, MHE. JANUARY MAKAMBA (Mb), KUHUSU UZINDUZI WA KIKOSI-KAZI CHA KITAIFA CHA BONDE LA MTO RUAHA MKUU 

Makamu wa Rais na Mawaziri Watano Kuelekea Iringa tarehe 11 Aprili 2017 Kuokoa Mto Ruaha Mkuu.

Bonde la Mto Ruaha Mkuu linakabiliwa na uharibifu mkubwa wa mazingira, hususan uharibifu wa mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji. Uharibifu huu unatokana na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu unaofanywa katika maeneo ya vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kwenye vilele vya milima, kwenye miteremko ya milima na katika mabonde.

Umuhimu wa Bonde la Mto Ruaha Mkuu

Bonde la Mto Ruaha Mkuu lina umuhimu wa pekee katika uchumi wa nchi yetu na duniani kwa ujumla kutokana na baadhi ya sababu zifuatazo:-
• Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye ukubwa wa kilometa za mraba 20,226 iliyo kubwa kuliko zote  Afrika Mashariki iko katika bonde la mto huu. Aidha Hifadhi hiyo ni sehemu ya mfumo mkubwa zaidi wa ikolojia yenye ukubwa wa zaidi ya kilometa za mraba 45,000 ikujumuisha hifadhi za wanyama za Rungwa, Kizigo, na Muhezi ambazo zote zipo ndani ya Bonde la Ruaha Mkuu.
• Shughuli mbalimbali za kiuchumi zinategemea bonde hili kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, wanyamapori na utalii.
• Huduma za kiikoloji (ecosystem goods and services) kama vile upatikanaji wa maji na unyonyaji wa hewa ukaa kupitia misitu ya hifadhi hutokana na kuwepo kwa bonde hili.
• Bonde hili linachangia kwa kiasi cha asilimia 80 ya uzalishaji wa umeme unaozalishwa kwa maji nchini kutoka mabwawa ya Kidatu na Mtera. Umeme huu, unaondesha shughuli za kiuchumi na kijamii, ni kutokana na kuwepo kwa bonde hili
• Bonde la Mto Ruaha Mkuu ndio mhimili, na ndilo linamwaga maji katika, Bonde la Kilombero na Bonde la Rufiji, ambayo huchangia zaidi ya asilimia 20 ya Pato la Taifa na hutegemewa na mamilioni ya Watanzania kwa shughuli za uzalishaji mali.

Ndugu wananchi,

Hali ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu

Hali ya mazingira katika Bonde la Mto Ruaha Mkuu ni mbaya sana. Mazingira yameharibika na kusababisha athari kubwa zinazotishia ustawi wa jamii, uchumi wa nchi na mifumo Ikolojia ya bonde hilo yenye umuhimu wa kidunia pia. Kupungua kwa mtiririko wa maji katika vijito na Mto Ruaha Mkuu ulijidhihirisha kuanzia miaka ya 90 ambapo shughuli mbali mbali za kibinadamu zisizo endelevu ziliongezeka. Kuanzia kipindi hicho maji yaliendelea kukauka kwa kasi kwa vipindi virefu vya hadi miezi sita kwa mwaka. Aidha, wakati wa kiangazi mto huu hukauka na maji hayafiki kabisa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Hali ya kupungua kwa maji imesababisha athari nyingi sana ikiwa ni pamoja na:
• Kukosekana kwa maji kwa ajili ya wanyama na mimea katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, jambo lililopunguza mvuto na mapato ya utalii lakini pia kuongeza ujangili kwasababu ya wanyama kutoka nje ya hifadhi;
• Kupungua kwa uzalishaji wa umeme katika mabwawa ya Mtera na Kidatu, hali iliyosababisha mgawo wa umeme na kuathirika kwa uzalishaji viwandani na biashara na shughuli nyingine za uchumi.
• Kupungua kwa idadi na aina ya wanyama, ndege , samaki, mamba na viboko.
• Upotevu wa bioanuai ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu kwa kiasi kikubwa na baadhi ya aina za viumbe hai kuwa katika hatari ya kutoweka.
• Ukame katika Bonde la Rufiji na kupungua kwa ukubwa wa misitu ya mikoko na uvuvi wa kamba, na
• Ukame katika bonde la mto Kilombero na kuathiri shughuli za kilimo (miwa na  mpunga )


Jitihada Mbalimbali Zilizochukuliwa

Ndugu wanahabari,

Kufuatia ongezeko la vipindi virefu vya kukauka kwa mto hasa kipindi cha kiangazi, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikifanya jitihada ya kukabiliana na changamoto hizo. Jitihada hizi zilianza miaka ya 1990 na zilihusisha kubuni na kutekeleza mikakati, mipango, programmu na miradi mbalimbali yenye lengo la kuboresha mazingira na mfumo ikolojia wa Mto Ruaha mkuu.

Katika utekelezaji wa mikakati, mipango, programmu na miradi mbalimbali kumekuwa na mafanikio ya hapa na pale. Hata hivyo, kiujumla bado changamoto za kimazingira ikiwa ni pamoja na kupungua kwa mtiririko wa maji katika  Mto Ruaha Mkuu zimeendelea kuongezeka. Tafsiri ya haya yote ni kwamba jitihada zote ambazo zimewahi kufanyika hazijaweza kuzaa matunda endelevu kwa kiwango cha kutosha.

Hatima ya Mto Ruaha Mkuu na Mtazamo wa Hatua Mpya

Ndugu Wanahabari,

Iwapo hali hii itaachwa iendelee kama ilivyo bila jitihada zozote zenye mtazamo mpya na za makusudi, ni dhahiri miaka michache ijayo Mto Ruaha Mkuu utakauka  na kupotea kabisa kama baadhi ya vijito hapa nchini. Na hili litakuwa ni janga kubwa kuliko majanga yote yaliyowahi kutokea hapa nchini.

Haja ya kuwa na Kikosi Kazi cha Kitaifa

Baada ya tafakari ya kina ya hali hii na kwa kuzingatia umuhimu wa eneo hili, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeona kuna haja ya kuwa na “mtazamo mpya” wa namna ya kukabiliana na changamoto za Mto Ruaha Mkuu kwa ufanisi zaidi.

Kwa muktadha huo, kwa mujibu wa mamlaka na wajibu niliopewa na Sheria ya Mazingira ya 2014, nimeunda Kikosi Kazi cha Kitaifa cha kunusuru ikolojia ya bonde la Mto Ruaha Mkuu kinachojumuisha viongozi, watendaji na wataalam katika sekta muhimu kitakachokuwa na jukumu la kuandaa “mtazamo mpya” wa kukabiliana na changamoto hizo, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za haraka na za dharura na pia kubuni mikakati, mipango na mbinu bora (innovative strategies) zaidi za kukabiliana na changamoto za Mto Ruaha Mkuu.

 Hitimisho

Kutokana na umuhimu wa suala hili kwa mustakabali wa taifa, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amekubali kuzindua Kikosi Kazi hiki na kuongoza kikao chake cha kwanza tarehe 11 Aprili 2017 mkoani Iringa, ili kulipa jambo hili uzito unaostahili kwa lengo la kuhakikisha kuwa mazingira na mifumo ikolojia ya bonde la mto Ruaha Mkuu yanarudia katika hali ya awali ili kutoa huduma inayostahili kwa jamii na nchi kwa ujumla kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho. Vilevile, mawaziri wanne ambao sekta zao zinahusika na suala hili watashiriki katika kikao hicho. Mawaziri hao ni Mheshimiwa William Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mheshimiwa Gerson Lwenge, Waziri wa Maji na Umwagiliaji; Mheshimiwa Dkt. Charles Tizeba, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi; na Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Maliasili na Utalii.

Kikosi-Kazi kitakuwa na Hadidu za Rejea zifuatazo:

1. Kuchambua kwa kina tafiti na matokeo ya miradi mbalimbali ya Serikali na wafadhili ambayo imeshafanywa katika Mfumo – Ilkolojia wa Mto Ruaha Mkuu na Ardhioevu (Wetland) ya bonde la Usangu na kubanisha hatua mpya na za haraka za kudhibiti kupungua kwa maji kwenye Mto ruaha Mkuu;

2. Kukusanya maoni na mapendekezo ya wadau wote, ikiwemo wananchi waishio katika bonde la Mto Ruaha mkuu, kuhusu hatua za hifadhi ya Mazingira katika bonde hilo;

3. Kutumia Mamlaka ya Sheria mbalimbali husika kuchukua hatua za haraka za kudhibiti uharibifu wa mazingira na kurekebisha madhara ya uharibifu wa mazingira yaliyojitokeza;

4. Kuandaa rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Hifadhi ya Mazingira ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu; na

5. Kutoa ushauri wowote wa kisera au kiutendaji wenye lengo la kuokoa mfumo – ikolojia wa bonde la Mto Ruaha Mkuu. 

Kikosi-Kazi kinatarajiwa kufanya kazi kwenye eneo la Bonde kwa kuchukua hatua za haraka zilizo chini ya mamlaka yao ya Kisheria. Vilevile, inatarajiwa kwamba mikakati na mapendekezo yatakayoainishwa na Kikosi-Kazi kwa ajili ya maamuzi ya kisera yatakabidhiwa kwa Makamu wa Rais mnamo tarehe 16 Mei 2017 kwa ajili ya kupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri na maamuzi hayo kufanyika.

Wajumbe wa Kikosi Kazi ni Wafuatao

Dkt. Andrew Komba,
Mkurugenzi,Uratibu wa Sera,
Ofisi ya Rais-TAMISEMI,
S.L.P 1923,
DODOMA.

Bw. Richard Muyungi,
Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira,
Ofisi ya Makamu wa Rais,

Mhandisi Seth Luswema,
Wizara ya Maji na Umwagiliaji,

Dkt. Stephen Nindi,
Kaimu Mkurugenzi Mkuu,
Tume ya Taifa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi,

Bi. Mary Makondo,
Kamishna wa Ardhi,
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,

Bw. Idris A. Msuya,
Mkurugenzi,
Bodi ya Bonde la Mto Rufiji,

Bw. Jackson Lesika Saitabau,
Katibu Tawala wa Mkoa,
NJOMBE.

Bibi Wamoja Ayubu Dickolagwa,
Katibu Tawala wa Mkoa,
IRINGA.

Bibi Mariamu Amri Mtunguja,
Katibu Tawala wa Mkoa,
MBEYA.

Dkt. Allan Kijazi,
Mkurugenzi Mkuu – TANAPA,
(Mhifadhi Ruaha),
ARUSHA.

Mhe. George M. Masaju,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,

Mhandisi Bonaventura T. Baya,
Mkurgenzi Mkuu,
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)

Dkt. Tito Mwinuka
Kaimu Mkurugenzi Mkuu
TANESCO


ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

Reactions:

0 comments:

Post a Comment