Thursday, 27 April 2017

RAILA ODINGA KUMVAA UHURU KENYETTA UCHAGUZI MKUU KENYA

Tokeo la picha la Raila Odinga kugombea urais

Muungano wa Vyama vya Upinzani nchini Kenya ‘National Super Alliance’ (NASA) umemteua aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga kuwa mgombea wake katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti mwaka huu nchini humo.

 Odinga sasa atakabiliana na Rais Uhuru Kenyatta atakayetumia chama cha Jubilee kuwania muhula wa pili.

“Hii ni heshima kubwa sana ambayo ndugu zangu wamenifanyia, kwa kuniweka nipeperushe bendera ya NASA. Tumekuwa na vikao ambavyo vimechukua siku nyingi. Kila kitu tumeandika, tumekubaliana ya kwanza serikali tutakayoiunda, ambayo ni serikali ya mseto itakuwa ni serikali ya mpito,” amesema Odinga.

Akihutubia mamia ya wafuasi wa NASA mara baada ya kutangazwa kuwa mgombea amesema atakuwa kama Joshua kwenye Biblia na kuvusha Wakenya hadi nchi ya ahadi.

 “Sisi tuko kama timu, yenye pembe tano (Pentagon), wamenipa utepe wa nahodha, hiyo inaniunganisha mimi, wao na Wakenya wote, tutatembea pamoja bega kwa bega. Tunataka kubadilisha Kenya na kutekeleza ndoto ya waanzilishi wa taifa letu,” ameongeza.

Amesema Serikali yake itajikita katika kumaliza umasikini, kuimarisha afya, kuboresha uchumi, kubuni nafasi za kazi na kurejesha gharama ya elimu na kuboresha maisha ya watu wa chini.

Odinga pia ameahidi kuhakikisha walimu na madaktari pamoja na wafanyakazi wengine wanalipwa mishahara mizuri na kumaliza tatizo la rushwa serikalini .

Naye Makamu wa Rais wa zamani, Musalia Mudavadi amesema viongozi wote wakuu wa muungano huo wamekubalina kumuunga mkono mgombea huyo mmoja.

“Tumekubali kwamba mpangilio huu wa uongozi ni mpangilio ambao tunataka ulinganishwe na Rasimu ya Bomas ambayo Wakenya waliitaka, lakini haikuidhinishwa,” amesema.

Mgombea mwenza wa Odinga atakuwa Makamu wa Rais wa zamani, Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Chama cha Wiper Democratic Movement.

Waziri Mkuu na Mratibu wa shughuli za Serikali atakuwa kiongozi wa chama cha Amani National Congress, Musalia Mudavadi. Naibu Waziri Mkuu na Mratibu wa Uchumi atakuwa kiongozi wa Ford Kenya, Moses Wetangula.


Kiongozi wa Chama cha Mashinani (CCM), Isaac Ruto atakuwa Naibu Waziri Mkuu atakayesimamia Utawala na Huduma za Jamii.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment