Monday, 24 April 2017

MKUU WA MKOA IRINGA AZINDUA WIKI YA CHANJO
MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amesema baadhi ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanakabiliwa tishio la aina mpya ya ukatili mkoani kwake unaowanyima haki ya kupata chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali hatari kwa maisha yao.

Aliyasema hayo katika mtaa wa Msisina pembezoni mwa Manispaa ya Iringa jana wakati akizindua kimkoa wiki ya huduma za chanjo, mkoani Iringa.

“Wazazi au walezi wanaozuia watoto kupata au kupuuza watoto wao kupata huduma ya chanjo, wanafanya ukatili,” alisema.

Alisema takwimu za mwaka 2016 zinaonesha watoto 2,243 sawa na asilimia sita hawakukamilisha chanjo ya kuzuia ugonjwa wa donda koo, kifaduro, pepopunda, homa ya ini, homa ya uti wa mgongo na ugonjwa wa kupooza.

Kwa upande wa chanjo ya surua, Masenza alisema takwimu hizo zinaonesha watoto 1,495 sawa na asilimia 4 hawakupata chanjo wakati watoto 5,979 sawa na asilimia 16 hawakupata dozi ya pili ya kukamilisha chanjo ya surua.

“Kwa takwimu hizi inaonesha watoto wengi hawakupata au kukamilisha chanjo zao kwa wakati na wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo,” alisema.

Alitoa wito kwa wazazi au walezi wenye watoto wa miaka chini ya mitano kutimia wiki hii ya chanjo kuwapaleka watoto wao katika vituo vya huduma ili wakapate huduma hiyo.

Awali Diwani wa Bashiri Mtove alimwambia mkuu wa mkoa kwamba kata hiyo yenye eneo kubwa la utawala kuliko kata zote za manispaa ya Iringa inakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma za afya.

“Kata hii ambayo ukubwa wake ni kilometa za mraba 162 ina Zahanati moja tu na kwa mfano watu wa mtaa huu wa Msisina ili wafike katika zahanati hiyo wanahitaji kutembea zaidi ya kilometa 12,” alisema huku akiomba msaada wa kupaua zahanati inayojengwa katika mtaa wa Mgongo.

Akiitikia ombi wa diwani huyo, Mkuu wa Mkoa aliahidi kuchangia Sh Milioni moja kwa masharti kwamba ni lazima zahanati hiyo iwe na chumba maalumu kwa ajili ya huduma ya mama na mtoto.

Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Iringa, Naftal Mwalongo alisema chanjo hizo zinatolewa ikiwa ni utekelezaji wa malengo endelevu ya dunia yanayohusu afya ambayo moja ya lengo lake ni kupunguza vifo vya watoto wa miaka mitano ifikapo mwaka 2020.


Mwalongo alisema kamati ya uendeshaji wa huduma za afya mkoa inazishauri halmashauri za wilaya zitenge fedha za kutosha kwa ajili ya chanjo katika mpango kabambe wa huduma za afya wa halmashauri.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment