Thursday, 20 April 2017

MASHINDANO YA MAGARI IRINGA KUTIMUA VUMBI APRIL 22
GERALD Miller na Ahamed Huwel ni baadhi ya madereva wakongwe wa magari nchini watakaomenyana kwenye mashindano ya mbio za magari Iringa za zaidi ya kilomita 300 yatakayotimua vumbi April 22 hadi 23.

Mashindano hayo yanayotarajia kushirikisha madereva 20 yanadhaminiwa na kiwanda kipya cha kutengeneza maji ya kunywa cha mjini Iringa cha Maji Mkwawa.

Akizungumza na wanahabari jana, Mwenyekiti wa Klabu ya Magari Iringa, Hammid Mbata alisema mashindano hayo yanafanyika ikiwa ni zaidi ya miaka 10 toka yafanyike kwa mara ya mwisho.

“Hapo katikati tulishindwa kuandaa mashindano hayo kwasababu ya kukosekana kwa udhamini madhubuti,” alisema.

Alisema mashindano hayo yanayotarajia kuleta wageni zaidi ya 200 mjini Iringa ni kichochea cha biashara, utalii na maendeleo ya jumla ya mkoa wa Iringa.

“Yatazinduliwa saa tano asubuhi ya April 22 na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza katika kiwanda cha Maji Mkwawa kilichopo eneo la viwanda la Ipogolo, mjini Iringa,” alisema.

Baada ya kuazinduliwa, Mbata alisema washiriki wataelekea uwanja wa Samora kuonesha mbwembwe zao kwa wapenzi wa mchezo huo na baadaye wataelekea Chuo Kikuu cha Iringa yatakakoanzia mashindano hayo.

Alisema siku ya kwanza mashindano hayo yatapita katika kijiji cha Kigonzile, Mgongo, Igingilanyi, Kiwele na kutokea Chuo Kikuu cha Mkwawa huku siku ya pili yatapita kijiji cha Wenda, Kikombwe, Tanangozi, Kalenga, Makongati, Kiponzelo, Ifunda, Mgama na Ihemi.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela aliwataka wananchi wa wilaya ya Iringa kuchukua tahadhari wakati wa mashindano hayo ya magari.

“Katika barabara zote ambazo magari hayo yatapita, tunaomba watu wasikatize kabla magari hayo hayapita lakini pia tunatoa wito kwa madereva wa bodaboda kutotumia barabara zitakazotumika wakati wa mashindano hayo,” alisema.

Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Steven Nyandongo alisema katika njia ambazo mashindano hayo yatapita kuna maeneo hatarishi yatakayodhibitiwa kwa usalama.

“Kama polisi tumejipanga kusimamia mashindano haya kikamilifu, tunataka yaanze salama na yamalizike salama; kwahiyo tunawataka wananchi kuchukua tahadhari na washiriki wa mashindano ni lazima wazingatie sheria za barabarani,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment