Thursday, 27 April 2017

MAJI MAPYA, MAJI MKWAWA KUINGIA SOKONI


SERIKALI imeipongeza familia ya mfanyabiashara Ahamed Huwel kwa kuitikia wito wa Rais John Magufuli wa kuifanya Tanzania nchi ya viwanda kwa kuanzisha kiwanda cha kisasa cha maji mjini Iringa yanayojulikana kwa jina la Maji Mkwawa.

Maji hayo yaliyoingizwa sokoni hivikaribuni yalizinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza wakati wa uzinduzi wa mashindano ya magari Iringa yaliyodhaminiwa na kiwanda hicho, wiki iliyopita.

Akizungumza wakati wa kutoa zawadi kwa washindi wa shindano hilo la magari Mkuu wa Mkoa alisema; “Uzalendo ni pamoja na kujivunia kile tunachozalisha.”

Alisema Ahamed Huwel ametekeleza kwa vitendo kauli ya Rais Dk Magufuli ya Tanzania ya Viwanda kwa kuanzisha kiwanda hicho cha kisasa, kilichobaki ni kwa wadu kumuunga mkono.

“Kazi imebaki kwetu wana Iringa, ni muhimu tukamuunga mkono kwa kuwa wa kwanza kuyatumia maji haya,” alisema huku akiyapigia debe maji hayo kwa watanzania wengine.

Masenza alisema mbali na kiwanda hicho kuchangia pato la Taifa, kinatarajia pia kutoa ajira za moja kwa moja kiwandani na zile za mtu mmoja mmoja, kampuni au taasisi zitakazokuwa zikifanya biashara ya maji hayo.

Msimamizi wa Uzalishaji wa kiwanda hicho, Kevin Robert alisema kiwanda hicho ambacho mpaka sasa kimekwisha ajili wafanyakazi 23 wa kudumu kina uwezo wa kuzalisha lita 28,000 kwa saa.


“Na kitakuwa kifanya kazi kwa saa nane kila siku hivyo kuzalisha lita 224,000 kwa siku zitakazojazwa kwenye chupa za ujazo tofauti kwa kuzingatia mahitaji na kipato cha mtu,” alisema.

Alisema Maji Mkwawa yataingia sokoni wakati wowote kuanzia sasa baada ya kiwanda hicho kukamilisha taratibu chache za uzalishaji zilizasalia.


Akizungumzia tofauti ya maji hayo na ya viwanda vingine, Robert alisema; “Maji Mkwawa ni salama kwasababu yanatoka chini ya ardhi na yanazalishwa kwa kutumia tekenolojia ya kisasa.”

Reactions:

0 comments:

Post a Comment