Saturday, 15 April 2017

LEMA AZUNGUMZIA ASKARI WALIOUAWA

Tokeo la picha la GODBLESS LEMA

Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, Godbless Lema ameeleza kusikitishwa kwake na tukio la mauaji ya askari wanane (8) lililotokea Mkoani Pwani hivi karibuni na kutaka idara za ulinzi na usalama kufanya utafiti wa kina ili kujua nini haswa sababu ya matukio kama hayo.

Lema ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), amesema hatuwezi kuishi kwa amani bila ya kuwa na Jeshi la Polisi imara na ili hilo lifanikiwe jamii inapaswa kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo haswa katika nyakati ngumu kama hizi.

“Ni matumaini yangu kuwa wananchi wote hususani wa maeneo hayo yalipotokea mauaji watakuwa tayari kutoa ushirikiano ili kuwabaini wahusika wa tukio hili baya,” amesema.

Ameongeza kuwa tukio la kuuwawa askari wa Jeshi la Polisi linapaswa kulaaniwa kwa nguvu zote na kila Raia wa Taifa letu kwani hiyo ni dalili mbaya kwa ustawi wa Taifa na kumuomba Mungu awatie nguvu ndugu, rafiki na familia zote za marehemu waliofikwa na msiba huo mbaya sana na mzito .


 “Polisi wameuwawa wakiwa kwenye wajibu wao wa kulinda raia na mali zao ni muhimu sasa kwa vyombo vya usalama kuwatia nguvuni na kuthibiti kwa weledi matendo kama haya yanayoendelea kushamiri kwa kasi sana, pia ni muhimu idara za ulinzi na usalama kufanya utafiti wa kina kujua ni nini haswa sababu za matukio kama haya” amesisitiza Lema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment