Monday, 10 April 2017

JET WATAKA MUENDELEZO HABARI ZA MIGOGORO YA ARDHI

Tokeo la picha la Deodatus mfugale

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kimesema habari za migogoro ya ardhi nchini zinatakiwa kuandikwa kwa weledi na ustadi mkubwa ili kuisaidia serikali na wadau wa sekta hiyo kuishughulikia kwa ufanisi.

Hayo yalisemwa na mwandishi nguri wa mazingira Deodatus Mfugale ambaye pia ni mkuu wa mafunzo wa JET kwenye mafunzo ya uandishi wa habari za mazingira, yaliyofanyika jijini hapa mwishoni mwa wiki.

Mafunzo hayo ya siku moja yalishirikisha baadhi ya waandishi wa habari za mazingira wanaofanya kazi katika wilaya tano za Rufiji, Kilwa, Kilolo, Mufindi na Mbarali ambako JET wanatekeleza mradi wa Ardhi Yetu Ajenda Yetu.

Mfugale alisema habari hizo hazitakiwi kuishia njiani na badala yake zinatakiwa kuwa za mfululizo ili ziweze kusaidia kuleta mabadiliko chanya yanayotakiwa.

“Tunachoshuhudia hivisasa katika vyombo vyetu mbalimbali vya habari ni kukosekana kwa mfululizo wa habari zinazoweza kuleta mabadiliko,” alisema.

Alisema JET inataka kuona waandishi wa habari wakiandika kwa kina zitakazowawezesha wadau wote kujua jinsi ardhi inavyoweza kuathiri maisha ya binadamu.

“Kwahiyo tumewakumbusha wanahabari walioshiriki mafunzo haya, namna ya kuandika habari za ardhi kwa usahihi na kwa wakati ili kupunguza na kumaliza migogoro iliyopo na inayotokea,” alisema.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo alisema migogoro mingi ya ardhi nchini imekuwa ikitokea kwasababu watu wengi wanakosa uelewa nwa mambo mbalimbali yanayohusu sekta hiyo, sera na sheria zake.

Alisema JET kwa kupitia timu kubwa ya wanahabari wa mazingira nchini kote inajitahidi kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu ardhi, migogoro yake na namna haki inavyoweza kupatikana kwa kupitia sheria zilizopo.

“Jet tunaataka kuona watu, taasisi au wawekezaji wanamiliki ardhi kihalali, vilevile wananchi wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu rasimali hiyo na thamani yake,” alisema.


Katika mafunzo hayo, Taasisi ya Utafiti wa Utetezi wa Haki Ardhi (Haki Ardhi) kupitia kwa mwanasheria wake Joseph Chiombola ilitoa ufafanuzi wa sera na sheria za ardhi na utawala katika muundo wa serikali za mitaa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment