Wednesday, 19 April 2017

DC MOFUGA AWAASA VIONGOZI WA SACCOS YA AKINAMAMA WA MBULU


MKUU wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga amewataka viongozi wa Saccos ya akinamama wa halmashauri ya mji wa Mbulu kuhakikisha wanakuwa wawazi na kutoa taarifa za hesabu za umoja huo kila wakati ili kuondokana na migogoro isiyo ya lazima.

Alitoa agizo hilo juzi mjini Mbulu wakati akizundua Saccos hiyo iliyoanza na mtaji wa Sh Milioni 41 unaotokana na hisa za wachama wake zaidi ya 50.

“Njia pekee ya kuufanya umoja wenu huu wa kuweka na kukopa udumu ni kuwa wawazi, waaminifu na mnaozingatia taratibu za uendeshaji mlizojiwekea ili mfikie malengo yenu,” alisema.

Alisema vyama vingi vya ushirika nchini vimekufa kutokana na viongozi wake kutokuwa waaminifu hivyo serikali itashirikiana nanyi ili suala hilo lisitokee katika umoja huo.

Mofuga alisema ni kwa kupitia vyama vya ushirika kama huo, ndiko ambako wananchi wenye kipato kidogo na cha kati wanaweza kupata mikopo ya kukuza mitaji yao.

“Kukuza mtaji maana yake ni kutanua shughuli ya kiuchumi unayofanya, na kwa kufanya hivyo unajiweka katika mazingira ya kulifikia soko kubwa zaidi na hatimaye utaongeza faida,” alisema.

Mkuu wa wilaya huyo alisema ni mategemeo yake kwamba akinamama wa wilaya hiyo, wataongeza kasi ya ushiriki wao kwenye shughuli za kijasiriamali kwa kupitia Saccos hiyo.

“Lengo la serikali ni kuona watu wake, wakiwemo wanawake wanakuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba na kuitumia akiba hiyo kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo ili kuinua uchumi wao,” alisema.

Aliwapongeza akinamama hao akisema, kasi waliyoanza nayo; wakiitumia vyema wanaweza kuwa na mtaji utakaowawezesha kuanzisha kiwanda kidogo cha usindikaji wa mazao ili kuchochea uzalishaji wake na kutanua soko la ajira.


Mofuga aliwashukuru pia wabunge wanaotoka wilayani humo akisema wanampa ushirikiano mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya serikali ikiwa ni pamoja na kuwahimiza wananchi kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment