Wednesday, 22 March 2017

WANAHABARI WATANGAZA KUSUSA HABARI ZOTE ZITAKAZOTANGAZWA NA MAKONDA

Tokeo la picha la neville meena

Sakata la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda Kuvamia kituo cha Clouds akiwa na Askari wenye silaha limeibua mapya hii leo baada ya Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF) kuvitaka vyombo vya habari vyote nchini kususa kuandika habari zake zinazohusu mikutano na wanahabari na shughuli mbalimbali za kiserikali anazofanya.

Taarifa ya Mwenyekiti TEF Theophil Makunga imelaani vikali kitendo cha Makonda cha kuvamia kituo cha Utangazaji cha Clouds usiku wa Machi 17 akiwa na askari wenye silaha.

“Tunamtangaza Ndugu Paul Makonda kuwa ni Adui wa Uhuru wa Habari, na yeyote yule atakayeshirikiana naye katika kukandamiza uhuru wa habari nchini,” ilisema taarifa hiyo ya TEF iliyoandikwa na Mwenyekiti wake, Theophil Makunga.

Katibu wa TEF, Neville Meena amewaonya wanahabari watakaokiuka msimamo huo akisema yatakayowakuta, hayatafanyiwa utetezi na Jukwaa hilo.

Aidha amefafanua kwamba Makonda ataendelea kuandikwa kwa habari zote zinazomtaka kutoa majibu kwa mambo mbalimbali yanayoendelea dhidi yake na yanayohusu maslai ya umma.


“Kwa mfano ameitwa na Kamati ya Bunge akitakiwa kwenda kujieleza kwa jambo lololote lile, hilo wahariri watakaa na kungalia namna ya kulifanyia kazi,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment