Thursday, 30 March 2017

UTAFITI WA ICISO KUTUMIKA KUBORESHA AFYA YA UZAZI NA MTOTO, KILOLO
HALMASHAURI ya wilaya ya Kilolo imeahidi kuutumia utafiti uliofanywa na Mwavuli wa Mashirika Yasio ya Kiserikali Mkoani Iringa (ICISO Umbrella) kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa huduma bora ya afya ya uzazi na mtoto.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri ya wilaya hiyo, Phillemon Naminga alisema changamoto nyingi zilizobainishwa kupitia taarifa ya utafiti huo zinasababishwa na pengo la mawasiliano na elimu ya utawala bora.

“Mtiririko wa kupeana taarifa kutoka chini hadi ngazi ya halmashauri ya wilaya sio mzuri, kuna pengo la namna ya kupena taarifa kati ya wananchi na viongozi na wakati mwingine viongozi wenyewe,” alisema.

Naminga alisema watautumia utafuti huo kutoa  elimu ya utawala bora katika ngazi zote za halmashauri, ili taarifa za changamoto zinazohusu upatikanaji wa huduma hizo na nyingine zifikishwe na kufanyiwa kazi kwa kuzingatia taratibu.

Akiwasilisha taarifa ya utafiti huo uliofanywa kwa miezi sita (Oktoba 2016 hadi Machi 2017) katika vijiji 40 vya kata ya Ibumu, Image, Idete, Irole, Ilula, Nyalumbu, Ruaha Mbuyuni, Uhambingeto na Nyanzwa Katibu Mtendaji wa ICISO, Raphael Mtitu alisema:

“Utafiti huo uliofadhiliwa na The Foundation for Civil Society ulilenga kuziwezesha asasi za kiraia na wananchi kutathimini na kupima matumizi ya fedha za umma katika serikali za mitaa juu ya ubora na uridhishwaji wa huduma zitolewazo, hususani kwenye afya ya uzazi na mtoto.

Mtitu alisema matokeo ya utafiti huo yanaonesha watu 319 sawa na asilimia 65 ya wahojiwa wote wameeleza uwepo wa huduma ya afya ya uzazi na mtoto katika maeneo yao na watu 172 walisema hakuna huduma hizo katika maeneo yao.

“Hiyo ni kwasababu ya kutokuwepo kwa vituo vya kutolea huduma katika vijiji vyao au wananchi na baadhi ya vijiji kuwa mbali na vituo vya kutolea huduma za afya,” alisema.

Akizungumzia umbali wa upatikanaji wa huduma, Mtitu alisema utafiti unaonesha zinapatikana kwa umbali wa kati ya kilimota moja na nne na zaidi ya kilomita tano huku miundombinu ya kufika katika baadhi ya vituo hivyo ikiwa mibovu.

Alisema utafiti huo unaonesha pia kwamba wananchi wanatumia wastani wa saa moja  hadi saa mbili kupata huduma hizo katika vituo vya kutolea huduma ingawa kuna baadhi wanatumia zaidi ya saa nne.

“Kuna haja ya kuwa na watoa huduma wa kutosha na vifaa tiba vya kutosha ili wananchi waweze kupata huduma kwa muda mfupi na kuwaepusha kwenda kwa waganga wa kienyeji au kujaribu kujitibu wao wenyewe,” alisema.

Alizitaja changamoto zingine zilizobainika kupitia utafiti huo kuwa ni pamoja na upungufu wa dawa, baadhi ya wananchi kutokuwa na elimu ya uzazi bora, ukosefu wa magari ya kubeba wagonjwa na tatizo la mawasiliano hasa kwa wajawazito na watoto wanaohitaji huduma za haraka.


Wakitoa maoni yao baada ya taarifa ya utafiti huo kuwasilishwa, wadau wa sekta hiyo waliiomba serikali iboreshe huduma hiyo huku vipaumbele vyao vikiwa ni huduma ya kliniki, usafiri kwa wajawazito, vifaa tiba, na huduma ya wakunga kabla na baada ya kujifungua.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment